CCM yaonya njama wabunge, madiwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza wabunge na madiwani walioko madarakani waache kupuuza majukumu yao kwa kisingizio cha maandalizi ya uchaguzi.

Kimesema kitafanya tathmini kwa kila mgombea kulingana na utendaji wake na si kwa uwezo wa kutoa fedha kwa wapiga kura.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ametoa msimamo huo Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makatibu wa matawi na kata wa Wilaya ya Dodoma.

“Tumeshuhudia watu wakichaguliwa lakini wanakaa miaka mitano bila kufanya kazi kwa sababu wanajua wapiga kura wachache wa ndani ya chama watakaowarudisha tena madarakani. Mfumo wetu mpya unalenga kumchagua mgombea kwa misingi ya kazi zake, si kwa kutumia rushwa au mbinu za kificho. Tunataka ukichaguliwa ukafanye kazi kwa wananchi,” amesema Dk Nchimbi.

Alisema mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, yalilenga kuongeza idadi ya wapiga kura katika kura za maoni ili kupata taswira pana ya maoni ya wananchi na kudhibiti mianya ya rushwa.

Aidha, CCM imeonya wanachama wanaotafuta uteuzi wa udiwani, uwakilishi na ubunge kwa njia zisizo halali na kimesema hakitasita kuwaengua watakaokiuka Katiba, Kanuni na maadili ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Tumeanza kuona matukio ya baadhi ya wabunge na madiwani wakipitisha fomu ili watangazwe kuwa wagombea
pekee. Wengine wanahamasisha vikao kutoa matamko kwamba wapitishwe bila kupingwa. Wapo wanaoandaa
kumbukumbu za misiba, siku za kuzaliwa na hata sherehe za ndoa, lakini wahudhuriaji wanapewa posho na wamevaa sare za CCM ili ionekane kama mkutano wa kisiasa,” alisema Dk Nchimbi.

Aliongeza: “Wapo wanaowapa posho wahudhuriaji wa mikutano wakiwa wamevaa sare za CCM ili kuonesha wanaungwa mkono. Tunawataka waache mara moja”.

Dk Nchimbi alisema CCM ina mfumo wa kufuatilia mwenendo wa wanachama wake na kumbukumbu zote
zinahifadhiwa.

“Wengine wameanzisha NGOs kwa malengo ya kisiasa, wengine wanatumia mbinu za kuwachafua waliopo madarakani kwa sasa.

Kwa wote hawa, tunasema waache mara moja. Wanapoteza muda na kutufanya tufikirie kuwaengua.  Hatutavumilia mambo haya,” alionya mtendaji huyo wa chama hicho tawala.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button