CCM yashinda udiwani Kigoma Ujiji
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kiti cha udiwani katika Kata ya Kasingirima Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya mgombea wa chama hicho Mlekwa Mfamao Kigeni kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye kata hiyo uliofanyika Machi 20,2024.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Mwantumu Mgonja kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi alimtangaza Mlekwa Kigeni wa CCM aliyeibuka mshindi baada ya kupata kura 437, huku minzani wake wa karibu Ahamad Alumbula wa ACT Wazalendo akipata kura 233. Vyama 12 vilisimamisha wagombea, ambapo vyama hivyo vingine hakuna mgombea aliyepita kura zaidi ya 10.
Msimamizi huyo wa uchaguzi amesema wapiga kura 713 walijitokeza katika uchaguzi huo, kati ya wapiga kura 1960 walioandikishwa, ambapo kura halali zilikuwa 699 na kura 14 zilikataliwa.
Uchaguzi huo mdogo umefanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Abdallah Kiembe aliyepata ajira ya serikali katika halmashauri ya Kondoa mkoani Dodoma.