Chalamila anusa hujuma mwendokasi

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema huduma za Kampuni ya Usafi ri wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ni mbovu na zinahujumu juhudi za serikali za kuboresha usafi ri kwa wananchi wa Dar es Salaam.
Chalamila amesema kampuni hiyo inahujumu juhudi za kisiasa, kiuongozi na juhudi za kutoa huduma za usafiri kwa wananchi.
Alisema hayo katika kituo cha mabasi ya mwendokasi Kimara Mwisho alipofanya ziara kukagua huduma za mabasi hayo jana asubuhi.
Chalamila alisema huduma za kampuni hiyo zimekuwa zikidorora tangu zilipoanzishwa miaka tisa iliyopita na wananchi wanakosa huduma bora ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi.
“Mradi wa awali wa mwendokasi ulikuwa na urefu wa kilometa 20 ukijumuisha barabara ya Kivukoni, Kimara na Gerezani uliogharimu Sh bilioni 613 na ulipoanza mabasi 200 yaliletwa lakini hadi sasa mabasi yanayofanya kazi yamepungua na kubaki 60 tu hali inayowaumiza wananchi,” alisema.
Chalamila alieleza kusikitishwa na hali duni ya mabasi yanayotumika akisema mengi yanaendelea kuharibika na wananchi wanapanda mabasi yanayovuja na mengine milango inafunguka hovyo.
“Mkataba wenu unasema nini kuhusu kubadilisha magari? Kwamba yatadumu miaka 20 bila kubadilishwa? Wakati Watanzania wanaendelea kunyeshewa mvua ndani ya magari? Hii ni dharau kwa wananchi. Haiwezekani,” alisema Chalamila.
Aliongeza: “Miaka tisa hamjabadilisha magari, hata mtu binafsi tu gari la miaka tisa limeshachakaa, lakini hili ni basi la abiria linakwenda linarudi, miaka tisa hamjawahi kubadilisha gari…mnasubiri mpaka gari linyeshewe ndani, livunje mavioo kila kitu halafu ninyi ndio muagize mabasi, hiyo si dharau kwa Watanzania? Hivi tukisema mnafaa kuendesha, mnafaa kweli UDART? Kwa sababu hii mwendokasi imepoteza hata ladha”.
Chalamila alisema kama huduma zitaendelea kuwa mbovu kama ilivyo sasa serikali haiwezi kuwavumilia na lazima kampuni hiyo iwajibishwe kwa kuwa imeshindwa kutoa huduma.
Alisema wananchi wanalalamika na wanapanda mabasi ya mwendokasi kwa kupitia madirishani kwa sababu huduma za Udart ni mbovu.
“Kwenye video clips nyingi zinazotembea, watu wanaingilia madirishani, video clips nyingi zinazotembea magari yameharibika barabarani, video nyingi zinazotembea watu wana kadi wamesimama kwenye vituo vya mabasi na mabasi yanafika yamejaa na kadi zao zina pesa,” alisema.
Aliongeza: “Lakini pia video clips zinatembea magari yanavuja, watu wananyeshewa mvua ndani wameshika miamvuli ndani. Hiyo ndio azma ya mheshimiwa rais tunakoelekea? Si kufuja mali za Watanzania hawa?”
Chalamila alisema kama UDART itakuwa miongoni mwa kampuni zilizopewa fursa ya kutoa huduma ya usafiri wa mwendokasi, yeye atapendekeza wasipewe kazi hiyo.
“Kama mtakuwepo tena kwenye hizi barabara ‘nitapropose’ (nitapendekeza) msipatikane kwenye hizi barabara kubwa kwa sababu mmeaminika kwa miaka tisa na hamjafanya chochote,” alisema.
Chalamila alisema utendaji wa Udart haulingani na matarajio ya wananchi lakini juhudi za kuimarisha huduma hizo zimeanza kupitia ushirikiano wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Alisema kampuni ya TransDar inatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu kwa kuingiza mabasi mapya 177 yatakayofanya safari katika maeneo yenye changamoto kubwa ya usafiri.
Chalamila alisema serikali imekamilisha mradi wa awamu ya pili wa barabara yenye urefu wa kilometa
20.3 kutoka Halmashauri ya Jiji hadi Mbagala Rangi Tatu na ujenzi unaendelea kwenye daraja la Kigogo unaogharimu Sh bilioni 363.6.
“Serikali imeingia ubia na sekta binafsi kuongeza ushindani. Tayari tumefikia makubaliano na Kampuni ya Mofat ambayo italeta mabasi 200 ya kisasa yenye urefu wa meta 18 yatakayotumia gesi. Kati ya hayo, mabasi 99 yatakuwa yamewasili nchini ifikapo Agosti 15 na yataanza kutoa huduma kabla ya Agosti 30,” alisema.
Chalamila alisema barabara yenye urefu wa kilometa 23.6 kutoka Halmashauri ya Jiji kupitia Tazara hadi Gongo la Mboto, ujenzi umefikia asilimia 85 na itakapokuwa tayari serikali itatangaza zabuni kumpata mtoa huduma ili kuongeza ufanisi.
Alisema ujenzi wa barabara ya Tegeta–Mwenge hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 30.1 umefikia asilimia 30 na ikikamilika itatangazwa zabuni kupata waendeshaji.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando alimshukuru Chalamila kwa kusikiliza kilio cha wananchi kuhusu usafiri.
“Adha hii ina athari ya moja kwa moja kwenye uchumi wetu. Wananchi wanachelewa kwenye maeneo yao ya kuzalisha kutokana na magari mengi kuharibika. Tunataka kujua ni lini changamoto hii itapatiwa suluhisho,” alisema Msando.



