Chalamila apiga marufuku utupaji taka Tabata Liwiti

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameziagiza kampuni zinazokusanya na kusafirisha taka katika eneo la Tabata Liwiti, Mtaa wa Mfaume, Wilaya ya Ilala, kuacha mara moja utupaji wa taka ovyo na kuzitaka kuzipeleka katika dampo lililotengwa, ikiwemo Pugu.
Chalamila amesema wananchi wanalipia huduma ya ukusanyaji na usafirishaji wa taka, hivyo kampuni yanayotekeleza jukumu hilo yanapaswa kuzingatia makubaliano na kuhakikisha taka zinapelekwa katika maeneo rasmi yaliyotengwa.

Amesema mkandarasi yeyote atakayebainika kumwaga taka katika eneo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufutiwa mkataba na kampuni yake kuondolewa katika utekelezaji wa huduma hiyo.
Amesema utupaji taka ovyo unaweza kuhatarisha afya za wananchi, kuchangia milipuko ya magonjwa kama kipindupindu na kuharibu mazingira, huku akibainisha kuwa eneo hilo lipo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Aidha, amewataka wakurugenzi wa halmashauri wanaosimamia wakandarasi wa usafi kuhakikisha wanawajibika ipasavyo na kuchukua hatua dhidi ya kampuni zinazokiuka masharti ya kazi.
Amewataka viongozi wa serikali za mitaa, wenyeviti na watendaji kuhakikisha maeneo yao yanalindwa dhidi ya utupaji taka ovyo, akisisitiza kuwa jukumu la usafi haliwezi kuachwa kwa viongozi wa mkoa na wilaya pekee.
Katika hatua nyingine, Chalamila ameelekeza wananchi watakaokamatwa wakitupa taka ovyo wapewe adhabu ya kufanya usafi katika maeneo machafu kwa muda utakaopangwa, badala ya kufungwa pekee, ili kuwajengea uelewa wa umuhimu wa kutunza mazingira.

Amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuboresha Bonde la Mto Msimbazi, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kutupa taka katika maeneo hayo.
Kutokana na hali hiyo, amezitaka wataalamu kutoka Bonde la Msimbazi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kukutana na kuweka mkakati wa pamoja wa kudhibiti tatizo hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema changamoto hiyo inachangiwa na baadhi ya viongozi na wakazi wanaoshinikiza makampuni kutupa taka katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa tatizo jingine ni baadhi ya watu wanaojihusisha na masuala ya mazingira pamoja na kamati zao kutoa vibali vya uchimbaji mchanga kiholela katika eneo hilo.



