Chama cha wanaume chazindua mizinga 130 ya nyuki

DODOMA; CHAMA cha Wazee Wanaume Tanzania Mkoa wa Dodoma (CCWWT) kimeishukuru serikali kwa ufadhili wa mizinga 130 ya thamani ya Sh milioni 16.5 kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.
Aidha, chama hicho kimeishukuru Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu Rasilimali kwa kushirikiana na serikali kuwapatia eneo la kutundika mizinga hiyo ya nyuki lenye ekari 1,500 katika eneo la Makutupora na Mzakwe.
Shukurani hizo zilitolewa na Katibu wa chama hicho, George Andalla kwa niaba ya chama hicho kwenye uzinduzi wa mradi wa ufugaji nyuki uliopo bonde la Makutupora na Mzakwe jijini Dodoma.
–
Andalla alisema kupatikana kwa msaada huo kutawakomboa wazee hao kiuchumi zaidi na wataondokana na mzigo wa utegemezi kwa kuwa utawawezesha kutoa ajira kwa upande wao na hatimaye kujipatia kipato cha kujikimu kwa wanachama wake.
Aidha, msaada huo kwa wazee hao utategemewa pia kutoa ajira hata kwa vijana ambao wengi hawana ajira na wapo mitaani wengine wakijiingiza kwenye vitendo viovu ambapo itawalazimu kuachana navyo baada ya kujiunga na mradi huo wa ufugaji nyuki.
Katibu huyo alisema pamoja na kupatiwa mizinga na eneo la kutundika mizinga hiyo, bado chama hicho cha wazee wanaume wanaomba ardhi hekari 5,000 kwa ajili ya kilimo cha zabibu, alizeti, mtama, ufuta, mbogamboga, matunda na mazao mengine.
Msemaji wa chama hicho, Ntemo Athumani na Mjumbe wa Baraza la Wazee, Omary Ndubonguru, wamewaomba wahisani kuwaangalia kwa jicho la pili kwa kuwawezesha miradi mbalimbali ili waondokane na tabia ya kuombaomba.
Walisema chama hicho kuna wataalamu na wasomi wa fani mbalimbali ambazo walikuwa wakitumikia serikalini na maeneo mengineyo na wakiwezeshwa watakuwa wameisaidia serikali kuinua pato la uchumi kwa kupitia miradi watakayowezeshwa.



