WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana ameipongeza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa jitihada za kutangaza vivutio vya utalii nchini huku akisisitiza kuwa hayo ndio maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza falsafa ya 4R.
Falsafa hiyo ni Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).
Dk Chana amesema hayo leo Novemba 22, 2024 wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) zilizopo jijini Dar es Salaam.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuitangaza nchi lakini nasisitiza lazima muwe na ushirikiano katika Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili twende kwa pamoja, muende uwandani na kuvijua vivutio vilivyoko katika taasisi zote,” Chana amesisitiza.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema kuwa TTB imejikita katika vipaumbele kadhaa ikiwemo kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa taasisi hiyo kwa kuwekeza kwenye mali za TTB na kuzalisha mapato kupitia Kituo cha Kutangaza Utalii Kiditali (DDMCC).