Chaumma yaahidi mambo matano siku 100 Ikulu

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema wananchi wakikichagua ndani ya siku 100 serikali yake itatunga sheria ya matumizi ya akili unde.

Ilani ya Uchaguzi ya Chaumma 2025-2030 imeeleza serikali yake itatunga sheria hiyo na itahusu matumizi ya akili unde katika shule na vyuo bila kuathiri masuala ya ubunifu na uwezo wa wanafunzi kufikiri upya ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayokua kwa kasi ulimwenguni.

Ilani imeeleza sheria hiyo itakuwa kwa ajili ya maendeleo ya watu wote na si kutumika kuwaadhibu watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini.

SOMA: CHAUMMA yaahidi mshahara 800,000, mchele kilo Sh 500

Pia, Chaumma imeeleza ikipewa ridhaa ya kuiongoza serikali ndani ya siku 100 itaunda tume ya ardhi kuchunguza mgogoro wa wananchi na mamlaka za hifadhi za taifa za wanyamapori.

Ilani imeeleza tume hiyo itaundwa ili kuondoa tatizo la mauaji ya wananchi wanaoishi au kupakana na mamlaka za wanyamapori au mamlaka za misitu na mamlaka nyingine zinazohusika na masuala hayo.

Chama hicho kimeeleza tume hiyo itachunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa muda mrefu imelitafuna taifa katika maeneo mbalimbali nchini bila kuwa na ufumbuzi wa kudumu.

Chaumma imeeleza katika siku 100, serikali yake itaanzisha na kuzindua mkakati wa mfumo bora wa lishe nchini kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wote wanapata lishe bora kuanzia kwa watoto wadogo katika ngazi ya elimu ya awali, wanafunzi shuleni na wagonjwa katika hospitali za umma.

“Mkakati huu utaitwa ‘Ubwabwa kwa wote’ kwa kuwa kuboresha mfumo wa lishe ni kuhakikisha kwamba taifa linaondokana na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe nchini,” imeeleza ilani.

Chaumma imeahidi ndani ya siku 100 itawasilisha bungeni muswada wa kufuta tozo zote zinazoathiri sekta ya kilimo na ufugaji kwa sababu tozo hizo zimeathiri mapato kwa wakulima na upatikanaji wa chakula bora na nyama nchini jambo litakalorudisha nyuma mkakati wa upatikanaji wa ubwabwa kwa wote.

Pia, chama hicho kimeeleza kitatunga sheria ya kuhuisha mfumo wa serikali za mitaa kimuundo na kimapato. Chaumma imesema itafanya hivyo ili kufanya marekebisho ya utaratibu wa tozo na mapato ya halmashauri na serikali kuu ili kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato na kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikali kuu.

Pia, chama hicho kimeeleza kitahuisha mfumo mzima wa serikali za mitaa na halmashauri ikiwemo kuziunganisha halmashauri za wilaya au manispaa ambazo hazina uwezo wa kujiendesha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button