Chaumma yaahidi mshahara 800,000, mchele kilo Sh 500

 

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeahidi kulipa watumishi wa umma kima cha chini mshahara Sh 800,000 baada ya makato ya kisheria.

Mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Salum Mwalimu akiwa na mgombea mwenza, Devotha Minja alisema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu katika viwanja vya Biafra mkoani Dar es Salaam jana.

Pia, Chaumma ilizindua Ilani ya Uchaguzi ikiwa na vipaumbele kadhaa kikiwemo cha kuhakikisha lishe kwa Watanzania inakuwa ajenda muhimu.

Mwalimu alisema serikali ya Chaumma imedhamiria kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi ili waondokane na hali ngumu ya maisha.

“Hivyo na watumishi hao watakuwa na wajibu kwa kufanya kazi kwa weledi na tutaweka vigezo vya upimaji ufanisi na mtumishi akiharibu kwenye eneo lake la kazi, hakuna kuhamishwa bali ataondolewa kazini na hasara aliyosababisha atailipa,” alisema.

Alisema chama hicho kimejipanga kuja na majawabu na si malalamiko na yote yatafanywa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.

Mwalimu alisema Chaumma itafanya uboreshaji kwenye sekta ya kilimo na kuondoa kodi za vyakula ili bei ya vyakula ipungue na kufanya wananchi wamudu kula milo mitatu kwa siku.

Alisema sekta ya kilimo itaimarishwa ili kuzalisha chakula cha kutosha na mchele utauzwa si zaidi ya Sh 500 kwa kilo.

“Ni kweli nchi ina rasilimali za kutosha, tuna ardhi yenye rutuba na mabonde mengi. Tutaboresha kilimo ili tulime kwa wingi vyakula na kuondokana na njaa kwenye taifa na shuleni watoto wapate ubwabwa mchana,” alisema Mwalimu.

Alisema serikali yake itatenga asilimia 15 ya bajeti yote ya serikali kuhudumia sekta ya afya nchini ili kuondoa changamoto zilizopo sasa za kuwahudumia wananchi.

Mwalimu alisema wajawazito wataondokana na adha ya kununua vifaa vya kujifungulia wanavyotakiwa kwenda navyo hospitalini kujifungulia.

Kwenye vifaa vya ujenzi, Chaumma imeahidi kupunguza kodi ili kuwezesha wananchi kujenga nyumba za kisasa na kuondokana na nyumba za tembe.

Alisema serikali ya chama hicho itapunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi 12 ili kupunguza gharama na kumuwezesha mwananchi kuwa na uchumi na kuondokana na umasikini.

Serikali ya chama hicho imeahidi kutumia asilimia 30 ya mapato ya madini kuwezesha biashara changa kukua kufika za kati, za kati kuwa kubwa na kubwa zikue zaidi ili waendeshaji wake wawe wawekezaji.

Kuhusu diplomasia, chama hicho kimesema kinaamini katika uraia pacha hivyo serikali ya chama hicho itaanzisha mfuko wa kuwasaidia diaspora.

Mwalimu alisema serikali ya Chaumma itafanya sekta ya habari kuwa mhimili kamili na kuwa kiunganishi cha mihimili mingine kwa sababu habari hulielezea taifa.

“Tumeamua kuiweka mbele kwa sababu ndio tunaamini itaeleza serikali ilivyo ili ionwe, serikali isiyokubali kuonwa ni serikali isiyo safi na mimi siogopi kumulikwa kwa sababu nakwenda kuongoza serikali iliyo safi ndani na nje,” alisema.

Aliongeza: “Ilani yetu inataka kila mmoja aheshimu sheria na hakuna atakayekuwa juu ya sheria, hata mimi nikikosea mamlaka husika inihukumu kwa sababu sitakuwa juu ya sheria”.

Mwalimu alisema wataboresha mazingira ya kufundishia na mwalimu mmoja atafundisha darasa la wanafunzi wasiozidi 45 sambamba na kuboresha na kuongeza madarasa na usafi wa mazingira.

Kwa upande wake mgombea mwenza, Minja alisema mabadiliko yanawezekana. Alisema ikiwa wananchi wataamua kwamba mwaka huu chama hicho kinashika dola, wataondoa mikopo ya kausha damu.

Minja alisema chama hicho kitahakikisha maendeleo ya vitu yanaenda sambamba na maendeleo ya watu hivyo hakuna haja ya Watanzania kuendelea kuwa masikini.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe aliwashukuru Watanzania waliojitokeza kwenye uzinduzi wa kampeni ya chama hicho.

Habari Zifananazo

4 Comments

    1. JOIN US Everybody can earn 250/h Dollar + daily 1K… You can earn from 6000-12000 Dollar a month or even more if you work as a part time job…It’s easy, just follow instructions on this page, read it carefully from start to finish… It’s a flexible job but a good earning opportunity. tab for more detail thank you……..

      HERE——————————————⊃⫸ http://Www.Cash43.Com

    2. Google paid $220 an hour on the internet. My close relative has been without labor for nine months and the earlier month her compensation check was 25k by working at home for 10 hours a day….. Everybody must try this job now by just use this link

      COPY THIS→→→→ http://Www.CartBlinks.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button