“Cheti cha ndoa muhimu”

TIMU ya wanasheria chini ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe imetoa angalizo kwa wanandoa kutopuuza cheti cha ndoa kwani ni muhimu kwa pande zote mbili.

Hatua hiyo inakuja baada ya kupita kwenye maeneo tofauti kutoa elimu ya msaada wa kisheria na kubaini asilimia kubwa ya watu ikiwemo vijana na wazee hawana vyeti vya ndoa bali wanaishi kwa mazoea na wenza wao.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Bufanka kata ya Bugelenga, Wakili wa kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Esther Safari amesema wanandoa wengi wanapoteza haki zao kwa kukosa cheti cha ndoa.

Amesema cheti cha ndoa ni muhimu kwa mme na mke kwani suala la kuishi pamoja kwa muda mrefu si kigezo pekee ambacho kinahalalisha ndoa bali kama hakuna cheti cha ndoa yanabaki kuwa makubaliano binafsi.

“Jamani hivi vyeti siyo lazima kuwe na ng’ombe na mchele mkapika wali, unaweza ukampoteza mke wako kwa sababu ya uzembe tu wa kwenda kusajili ndoa yako jitahidi uirasimishe.

“Pia kwa mipango ya Mungu inaweza ikatokea akatangulia mmoja kati yenu, kuna mafao au kuna mali fulani baba au mama anaziacha, lakini ili upewe inahitaji uthibitisho wa kujua nani aliyekuwa mwenza halali wa huyu mtu.

“Akitokea mtu akapeleka cheti kwa mlango wa nyuma, na wewe ukaenda kwa barua ya mtendaji kwamba wewe ndio mke au mme atakayetambulika ni mwenye cheti cha ndoa”.

Wakili Esther amesisitiza uwepo wa vyeti vya ndoa vinasaidia kuepusha migogoro ya kifamilia pamoja na kumsaidia mke kupata haki za mmewe kazini hususani bima ya afya.

Ameongeza kuwa cheti cha ndoa kinatoa muongozo kwa mme kuongeza mke ama kubaki na mke mmoja kulingana na aina ya ndoa aliyosaini ama kuichagua kwenye cheti kama ni mke mmoja ama ndoa ya mitala.

“Sasa huyu baba ikitokea ana cheti ambacho alitiki ni mke mmoja akipata mke mwingine anakosea, kama unataka kuwa na wake wengi kafunge ndoa utiki pale cheti kinaposema hii ndoa itakuwa ya mitala.

“Hivi vyeti vinatolewa makanisani, vinatolewa misikitini, vinatolewa serikalini lakini cheti ni hicho hicho cha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hiyo kwenye kile cheti sasa wewe utachagua unataka ndoa gani”, amesema.

Mkazi wa kijiji cha Bufanka, Mashiku Salim amekiri kuwa umuhumu wa cheti cha ndoa ni mkubwa hasa kwenye kufanya maamuzi yenye manufaa kwa wanandoa wote lakini vijana wengi hawana kwa sababu ya uelewa.

“Wengine hawaoni umuhimu wa vyeti vya ndoa kwa sababu njia nyingi za utafutaji zinaibuka, kwani wanawake wengine wanatumia vyeti vya ndoa kudhulumu wanaume,

“Anaenda kuolewa lakini kwa sababu mwanaume ana mali anatumia cheti kama nyenzo ya kupata mali au mwanaume anaenda kwa mwanamke ambaye anakipato zaidi cheti anakitumia kama nyezo ya kupata mali” alisema Mashiku.

Naye Simon Daudi amesema vijana wengi hawana vyeti vya ndoa kwa sababu wanatumia njia ya mkato kuoana, ambapo wanaoana lakini wanakuwa hawana mapenzi ya dhati, ndoa zinadumu muda mfupi wanaachana.

“Kwa elimu hii iliyotolewa, kuna mitazamo ambayo wataiacha na kuona kumbe kupata cheti cha ndoa ni cha muhimu sana ukiwa kwenye ndoa”, amesema Simon.

MWISHO

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button