Chief Godlove: Vijana wekezeni katika ufugaji

DAR ES SALAAM: MFANYABIASHARA Godlove Mwakibete maarufu kama Chief Godlove, amewashauri vijana nchini Tanzania kuachana na fikra za kutegemea ajira pekee na badala yake kuanza kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali hususani ufugaji wa mifugo akieleza kuwa sekta hiyo ina fursa kubwa za kiuchumi ikiwa itasimamiwa kwa uvumilivu, maarifa na kujituma.
Akizungumza kuhusu maisha yake nje ya shughuli za kikazi Chief Godlove amesema yeye ni mpenzi wa ufugaji ambaye amekuwa akifuga nguruwe, ng’ombe wa nyama ng’ombe wa maziwa na farasi kwa sababu ya kupenda wanyama, akibainisha kuwa alianza ufugaji kwa mapenzi binafsi badala ya lengo la kibiashara.
Hata hivyo amesema mifugo yake imeongezeka kwa kiwango kikubwa, hali inayomfanya sasa kufikiria kuingia rasmi katika biashara ya kuuza mifugo au kuanzisha mabucha ya nyama.
Amesema kwa sasa anafuga takribani nguruwe 500 idadi ambayo imeongezeka kutokana na uzazi wa mifugo hiyo huku nguruwe mmoja akiwa na uwezo wa kuzaa watoto wengi kwa mara moja kulingana na matunzo na mazingira ya ufugaji.
Ameeleza kuwa ongezeko hilo limemfanya aanze kutafakari namna bora ya kuendesha ufugaji huo kibiashara ikiwemo kupunguza baadhi ya mifugo na kuongeza maeneo ya malisho ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Akitoa ushauri kwa vijana wanaotaka kuingia katika sekta hiyo, Chief Godlove amesema ufugaji unaweza kuwa chanzo cha kipato na uwekezaji wa muda mrefu, akiwataka vijana kuanza na mifugo michache kulingana na uwezo wao badala ya kusubiri mpaka wapate mitaji mikubwa. Amesisitiza kuwa kijana mwenye eneo hata la ukubwa wa ekari moja anaweza kutafuta aina ya mifugo inayofaa mazingira yake ya kama nguruwe au mbuzi na kuanza kujenga msingi wa biashara hatua kwa hatua.
Aidha amewashauri vijana wenye maeneo ya malisho kuangalia fursa ya kununua ng’ombe waliokonda kuwanenepesha kwa kutumia chakula kinachofaa na kisha kuwauza kwa bei ya juu.
Kwa mujibu wa maelezo yake biashara hiyo inaweza kuwa na faida endapo mfugaji atapata mifugo kwa bei nzuri atadhibiti gharama za chakula na matunzo, na atakuwa na soko la uhakika la kuuza mifugo hiyo.
Chief Godlove ameeleza kuwa ufugaji wa nguruwe nao una fursa kubwa kutokana na uwezo wao wa kuzaa zaidi ya mara moja kwa mwaka akibainisha kuwa mfugaji anayezingatia lishe bora usafi na huduma za mifugo anaweza kuongeza idadi ya mifugo yake na kukuza biashara kwa muda.
Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa vijana kujifunza mbinu sahihi za ufugaji na kuzingatia gharama za chakula matibabu na uendeshaji kabla ya kuanza uwekezaji huo.
Katika hatua nyingine mfanyabiashara huyo amewataka vijana kubadili vipaumbele vya matumizi ya fedha zao akisema baadhi yao hutumia kiasi kikubwa cha fedha kununua simu za gharama na kugharamia maisha ya anasa huku wakipuuza fursa za kuanzisha miradi inayoweza kuwaingizia kipato.
Amesema badala ya kutumia fedha zote katika matumizi ya muda mfupi vijana wanaweza kutenga sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kununua mifugo na kuikuza hatua kwa hatua.
Amesisitiza kuwa ufugaji unahitaji uvumilivu, nidhamu, kujituma na maamuzi sahihi akieleza kuwa mifugo inaweza kuwa uwekezaji wa kudumu unaoweza kurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
Amewahimiza vijana kuanza na kile walicho nacho kutafuta elimu ya ufugaji na kuweka malengo ya muda mrefu, akisisitiza kuwa mafanikio ya kiuchumi hayaji kwa siku moja bali kwa kutumia muda na rasilimali zilizopo kujenga miradi endelevu.



