DAR ES SALAAM: Wizara ya Afya imeeleza umuhimu wa kuwa na chombo huru kitakachokuwa na jukumu la kutoa ithibati na kudhibiti ubora wa huduma za afya zinazotolewa nchini ili kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na kukuza utalii tiba nchini.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na katika ufunguzi wa kongamano la siku moja la wataalam wa afya wa Tanzania na Uingereza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Grace Magembe amewapongeza taasisi ya TUHEDE ambao ni watanzania wanaoishi nchini Uingereza (Diaspora) ambao wanashirikiana na na Taasisi zetu za Afya hapa nchini katika mafunzo, tafiti na ubunifu ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika tiba.
“Suala hili litapelekea huduma zetu za ubingwa na ubingwa bobezi kuboreka na hivyo kuwezesha nchi yetu kuwa kitovu cha tiba utalii kwa nchi zinazotuzunguka.
Dk Maghembe amewaomba wataalamu hao sana pamoja na maeneo hayo ambayo wameanza kushirikiana, washirikiane nao pia katika kuandaa miongozo na hatimae chombo ambacho kitakuwa na jukumu la kutoa ithibati ya utoaji wa huduma za afya kwa lengo la kudhibiti ubora wa huduma za afya nchini kama wanavyofanya nchini Uingereza.
” Nimesikiliza mada ya mtaalamu kutoka Uingereza ambae ameeleza namna mfumo wa ithibati na udhibiti ubora wa huduma za tiba unavyofanyika na namna wanavyochukua hatua stahiki nikaona na sisi tunaweza kufanya hivyo”.
Amesema tayari zipo taasisi na mabaraza ambayo yanafanya kazi hiyo lakini bado kuna maboresho yanayotakiwa kufanyika kwa lengo la kujiweka katika nafasi ya juu zaidi kwa.kufuata vigezo vya kitaifa na kimataifa.
Ameongeza kuwa “Tunahitaji kuwa na chombo huru kitakachotuambia hapa tunafanya vizuri na hapa hatufanyi vizuri, kwa lengo la kuboresha huduma zetu zaidi na zaidi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili(MOI) Dk Lemeri Mchome amesema mashirikiano haya ni endelevu kwasababu katika afya kila siku mambo mapya yanatokea, huduma mpya zinatokea,tiba na vipimo vipya na teknolojia inakwenda mbele.
Dk Mchome amesema sasa kuna matumizi ya akili bandi katika matibabu na kutoa huduma za kiafya bila matibabu hayo hawawezi kwenda mbele.
“Katika kongamano hili tuna mambo ya kushiriki moja ni kujifunza wenzetu wamefanyaje kule na pili kuona sisi tulichofanya na kufikia kuona changamoto na baada ya hapo tutakaa meza moja kuona namna tunatatua hayo mapungufu chini ya wizara ya afya kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa wananchi.