Chongolo ataka madeni ya wazabuni yalipwe Songwe

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameziagiza halmashauri za wilaya mkoani humo kuhakikisha zinalipa madeni ya wazabuni na watumishi yaliyokaa zaidi ya miaka minane kwa baadhi ya halmashauri tangu watoe huduma, hali inayosababisha malalamiko mengi.
Chongolo alisema katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa (RCC) kilichofanyika hivi karibu kwa ajili ya kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema anaumizwa na kitendo hicho cha wazabuni kucheleweshewa stahiki zao baada ya kutoa huduma kwa halmashauri.
Aliitolea mfano Halmashauri ya Mji Tunduma inayodaiwa Sh bilioni 1.8 na wazabuni pamoja na watumishi tangu 2019, hali iliyosababisha malalamiko mengi.
Alisema halmashauri zilihitaji huduma kwa sababu zilikuwepo kwenye bajeti zao, lakini hali imekua tofauti baada ya wao kuhudumiwa. “Lipeni madeni ya watu, miaka nane mzabuni anadai hela yake ninyi mnatoa visingizio vingi visivyo na maana, tusijijengee laana isiyokuwa na maana.
“Sisi tumepewa kazi ya kuwainua wafanyabiashara kuwa mabilionea na si kuwatengenezea mazingira mabaya ya kwenda kufilisika, “ alisisitiza Chongolo.
Alisema wazabuni hao walitoa huduma kwa nia njema, lakini sasa wanakumbwa na hali ngumu, ikiwa ni pamoja na kushindwa kulipa mikopo yao benki.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati ya RCC wa Songwe wamepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 na mkoa huo unataraja kukusanya Sh bilioni 231.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.59 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2024/2025.
Katika bajeti hiyo, matumizi ya kawaida yanakadiriwa kuwa Sh bilioni 165.3 na Sh bilioni 130.3, zikielekezwa katika malipo ya mishahara kwa watumishi.



