CMSA yataka tija mifuko ya uwekezaji mitaji na dhamana

DAR ES SALAAM; Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema itaendelea kusimamia vyema mifuko ya uwekezaji wa mitaji na dhamana nchini ili ijiendeshe kwa tija na kukidhi matakwa yake ya kuchochea maendeleo kwa jamii.

Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa soko wa CMSA, Exaut Julius aliyasema hayo Dar es Salaam alipomwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama katika uzinduzi wa mifuko mitatu ya uwekezaji wa Kampuni ya Itrust Finance Limited, ambayo ni mfuko wa kifedha, madini na nishati na mawasiliano.

Alisema kupitia mifumo hiyo ya usimamizi wawekezaji watapata faida ya uwekezaji, hivyo CMSA, itahakikisha inaisimamia vyema itekeleze shughuli zake kwa mujibu wa sheria na kanuni kutimiza matakwa yake ya kutoa faida na kuongeza thamani ya uwekezaji.

“Tunaipongeza Itrust kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuimarisha uwekezaji wa kidijitali nchini na sisi tutaendelea kuwasimamia vyema, kwani kupitia mifuko hii ya uwekezaji jamii itanufaika na itasaidia kuchangia katika sera ya serikali kukuza uchumi hususan kuwezesha wananchi wa hali ya chini,”alisema Julius.

Alieleza kuwa Mamlaka hiyo inaamini kuwa uwekezaji katika mifuko hiyo itaendeshwa kwa tija kutoa faida zaidi kwa wawekezaji na jamii kwa ujumla kukidhi takwa hilo la kisheria.

“CMSA itaendelea kutekeleza na kusimamia utekelezaji wa mikakati yenye lengo la kuchagiza maendeleo ya masoko ya mitaji kujenga uchumi shindani na kuchangia maendeleo ya watu,”alisema.

Naye Meneja wa Mifuko wa iTrust Finance Limited, Francis Samkyi alisema kampuni imeweka lengo la kukusanya Sh bilioni 10 kwa kila mfuko, huku ikitarajia kupata uwekezaji unaozidi kiwango hicho kutokana na mwitikio wa wawekezaji.

“Hivi ni vyombo vipya vinavyoweza kusaidia jamii ya Tanzania na kila mwekezaji anayetaka kuwekeza barani Afrika,” alisema Samkyi.

Alisema mifuko hiyo itawapa wawekezaji fursa ya kupanua wigo wa uwekezaji wao nje ya nchi wanazoishi, huku akifafanua kuwa kampuni haiwezi kutaja kiwango maalumu cha faida kitakachopatikana kwa kuwa bei za hisa hubadilika kulingana na mwenendo wa soko.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button