Congo yatoa shukrani mkutano wa SADC.EAC

CONGO : SERIKALI ya DRC imetoa shukrani kwa mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambao ulitoa taarifa ya pamoja ikizitaka nchi za miungano hiyo kuheshimu uhuru wa DRC na kuendeleza mpango wa kuondoa vikosi vya kigeni ambavyo havijaidhinishwa kutoka kwenye ardhi ya Congo.

Hatua hii inawalenga vikosi vya Rwanda na washirika wao wanaoendesha shughuli zao ndani ya mipaka ya DRC. Serikali ya DRC imesema, “Kujitolea kumaliza uwepo wowote wa kijeshi ambao haujaalikwa ni hatua muhimu katika juhudi za kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.”

Katika mkutano huo, hatua kadhaa za dharura zilipitishwa, zikiwemo, kukomesha vita na uhasama bila masharti,uwasilishaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu na kurudisha miili ya waliofariki na kuhamisha waliojeruhiwa.

Hatua zingine ni kuhakikisha usalama katika njia muhimu za usambazaji bidhaa, kama barabara na maziwa, kufungua tena Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma na kuhakikisha usalama katika mji wa Goma na maeneo ya jirani.

Serikali ya DRC pia ilisisitiza umuhimu wa kuendeleza michakato ya Luanda na Nairobi kama njia kuu za kutatua migogoro katika ukanda wa Maziwa Makuu. SOMA : Tanzania yazihakikishia EAC, SADC ushirikiano suluhu DR Congo

Mchakato wa Luanda unalenga kuhamasisha vikundi vyenye silaha kama Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) kuondoka nchini DRC na kuhakikisha vikosi vya Rwanda vinaondoka.

Pia, mchakato wa Nairobi unalenga kuwashirikisha watendaji wasio wa serikali katika majadiliano ya kuleta amani katika kanda.

Serikali ya DRC imetoa wito kwa wadau wote, ikiwa ni pamoja na wadau wa ndani na kimataifa, kutimiza wajibu wao na kutekeleza kwa uaminifu hatua zilizokubaliwa na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya makubaliano hayo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button