COPRA yakabidhi tani 1.5 za mbegu ya kisasa Mwanza

MWANZA: MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imekabidhi Mbegu ya kisasa ya Choroko tani moja na nusu kwa Wakulima wa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kuzitumia katika msimu wa kilimo wa 2025 ambapo zitasaidia kuongeza uzalishaji. 
Akiongea katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza leo tarehe 24 Oktoba, 2025 Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Chagu Ngh’oma ameishukuru taasisi hiyo na akatoa wito kwao kuwatafutia masoko wakulima ili walime kwa manufaa.

Ngh’oma amesema choroko kwa kipindi kirefu limekua ni zao la chakula na kidogo biashara hususani katika wilaya za Kwimba na Misungwi ila ujio wa taasisi hiyo na mikakati yake unatarajiwa kuleta manufaa kwa wakulima kuzalisha zaidi na kuuza na hatimaye kukuza hata uchumi wao.
Ameongeza kuwa kwa msimu wa 2024/25 mkoa wa Mwanza ulipanga kupata tani 30,000 za choroko ila ulipata tani 27,000 sawa na 73% kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo ya mbegu duni ila ujio wa mbegu hiyo ya kisasa utasaidia kufikia malengo kwani wakulima watakua na uhakika wa uzalishaji.

Aidha, amewataka wataalamu kuanzia ngazi za chini (maafisa Ugani) kusimamia ipasavyo ili kufikia malengo yaliyopangwa na kwamba itasaidia pia kuongeza mapato ya halmashauri kutoka kwenye zao hilo huku akibainisha kuwa kwa mwaka 2024/25 Kwimba ilikusanya Sh milioni 300 na Misungwi ikijikusanyia milioni 70.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Maendeleo ya Mazao ja Viwango COPRA Pendo Bigambo amesema taasisi hiyo imetoa mbegu hizo ili kuchagiza uzalishaji na amewataka wasimamizi kuzigawa mbegu hizo kwa kufuata muongozo wa mfumo ili kuwa na usawa.

Ameongeza kuwa kwa kanda ya Ziwa taasisi hiyo kinara wa usimamizi mifumo ya uzalishaji na usimamizi wa mazao kwa mwaka huu imetoa tani 192 ya mbegu bora za zao hilo ili kusimamia uzalishaji, uchakataji na kwamba itahakikisha mkulima anapata soko la uhakika wa mazao.



