CP Kombo:Uchaguzi utakuwa wa amani

ZANZIBAR : JESHI la Polisi Kamisheni ya Zanzibar limewahakikishia wananchi kuwa hali ya ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 inaendelea kuwa shwari.
Kamishna wa Polisi Zanzibar Kombo Khamis Kombo amesema jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama wa hali ya juu, na kuwataka wananchi washiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi bila hofu wala wasiwasi.
Kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, Tume ya Uchaguzi, vyama vya siasa na wadau wa amani, Jeshi la Polisi limeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Mikakati hiyo inahusisha kutoa ulinzi wa kutosha katika vituo vyote vya kupigia kura, kusimamia sheria kwa haki bila upendeleo, pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na kuepuka uchochezi au vurugu za kisiasa.
Aidha, Kamishna wa Polisi amesisitiza kuwa jeshi hilo halitavumilia mtu yeyote au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga amani au kuhamasisha maandamano haramu. SOMA: Wanakijiji wahimizwa ushirikiano na Polisi kuimarisha usalama
Amehimiza viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao kufuata sheria, kuheshimu mamlaka za uchaguzi na kuendeleza siasa za amani. “Amani ya Zanzibar ni ya thamani kubwa, tuilinde kwa pamoja ili Uchaguzi Mkuu 2025 uwe wa mfano wa demokrasia, utulivu na heshima ya sheria,” amesema Kamishna.



