CRDB wakabidhi madawati 150 Mbulu

MANYARA: Benki ya CRDB imekabidhi madawati 150 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Babati mkoani Manyara ili kukabiliana na upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari.

Hatua hiyo ni muendelezo wa jitihada za benk hiyo kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu bora na kuwa na mazingira bora ya kujifunzia.

Ili kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo, Benki ya CRDB imekabidhi madawati 50 kwa Shule ya Msingi Mahinge yenye jumla ya wanafunzi 600 na madawati 100 kwenye Shule ya Secondari ya Manyara Boys wilayani Babati mkoani Manyara.

Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kupitia mradi wa Keti na jifunze unaotekelezwa na Benki ya CRDB katika maeneo mbalimbali nchini baada ya utafiti kufanyika na kubaini upungufu wa madawati 300,000 nchi nzima na program hii amesema Inatekelezwa nchi nzima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli, amesema wilaya hiyo ina jumla ya shule 101, zikiwa na upungufu wa madawati unaotofautiana kulingana na idadi ya wanafunzi, wanaendelea kufanya jitihada ili kumaliza hali hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, ameipongeza Benki hiyo kwa kuunga mkono jitihada za serikali, akibainisha kuwa serikali kuu imetoa shilingi milioni 88.6 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Mtatifikolo na  Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya babati Godfrey Balaza wameishukuru Bank ya CRDB kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia lakini pia kwa kushirikiana nayo katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button