Daktari aeleza hatari maumivu ya kifua

MKURUGENZI wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Dk Tulizo Shemu amesema changamoto za maumivu makali upande wa kushoto wa kifua wakati mwingine hutokana na tatizo la mstuko wa moyo.

Kutokana na hili amewashauri jamii kufika hospitali mapema kwa ajili ya uchunguzi na kubaini chanzo cha tatizo moja kwa moja.

Amezungumza hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akiongea na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliofika kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika Kliniki ya JKCI iliyopo Kawe jijini Dar es Salaam.

Advertisement

“Watumie vyombo hivyo kuihamasisha jamii kufanya uchunguzi wa afya upande wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo,”amesisitiza.

Dk Shemu amesema magonjwa ya moyo yanaua kwa kasi hivyo jamii ikiweza kupata elimu ya kutosha ya namna ya kutambua na kujikinga na magonjwa hayo itaweza kuyadhibiti kwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

“Uchunguzi utasaidia kufahamu mapema na kuzuia gharama kubwa za matibabu ambazo mtu angetumia kwa kuchulewa kufanya uchunguzi.

Ameongeza “Magonjwa ya moyo huja kwakushtukiza, zaidi ya asilimia 60 ya watu wanaopata mstuko wa moyo hupoteza maisha kutokana na kuchelewa kupata huduma za matibabu kwa wakati”, amesema Dk. Shemu

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kuwa na maono ya kuwafikia watu wa aina mbalimbali kuwafanyia uchunguzi wa afya kwani bila hamasa hizo wapo watu ambao hasingepima.

Balile amesema kupitia upimaji huo wahariri zaidi ya 50 wamekutana kwaajili ya kuangalia afya zao ambapo wapo ambao hawakuwahi katika maisha yao kupima kipimo cha moyo hivyo kwao kuwa fursa.

“Kwakweli sisi kama wahariri tumefurahi sana kuona taasisi hii inatujali hivyo kuweka historia kubwa katika maisha yetu kwa kufanya vipimo hivi na kupata elimu ya kuwa tunachunguza afya zetu” amesema Balile

Aidha Balile amevitaka vyombo vya habari kuendelea kutumia vizuri kalamu zao kufikisha elimu sahihi kuhusu afya kutoka kwa wataalamu wa magonjwa mbalimbali hasa magonjwa yasiyoambukiza.