Jamii yahamasishwa kuchangia damu

KIGOMA: Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Damas Kayera ameihamasisha jamii kujenga utamaduni wa kuchangia damu mara kwa mara ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo katika hospitali na vituo vya afya.

Dk Kayera ameyasema hayo leo Mei 29, 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Makere wilayani Kasulu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyokwenda sambamba na zoezi la uchangiaji damu salama.

Amesema damu inayochangiwa imeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wajawazito, watoto pamoja na majeruhi wa ajali, huku akisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo muhimu la kibinadamu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wauguzi kupata stahiki zao kwa wakati ili kuongeza motisha wa kazi na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Makere, Samweli Kadogo amesema ushiriki wa watumishi wa afya katika uchangiaji damu unatoa hamasa kubwa kwa wananchi kushiriki zoezi hilo kwa hiari.

Naye, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Esta Kondo amesema wauguzi wameamua kuadhimisha siku yao kwa vitendo kupitia huduma kwa jamii ikiwemo uchangiaji damu kama sehemu ya kuenzi taaluma yao ya kuokoa maisha ya watu.

Katika maadhimisho hayo, baadhi ya wauguzi walitunukiwa beji na zawadi mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika sekta ya afya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button