Dar City, Srelio kazi ipo leo

LIGI Mkoa wa Dar es Salaam hatua ya robo fainali inatarajiwa kuanza leo usiku ambapo Dar City itachuana na Srelio kwenye Uwanja wa Don Bosco Oysterbay Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama Cha Basketball Dar es Salaam Haleluya Kavalambi, maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kuhimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo.

Advertisement

Dar City imemaliza mzunguko wa mechi 30 ikiwa kinara kwa pointi 57 huku Srelio ikimaliza katika nafasi ya nane kwa pointi 44 hivyo huenda mchezo ukawa wenye ushindani kutegemea na hatua waliyopo.

Atakayefuzu hatua ya nusu fainali ni yule atakayeshinda michezo miwili kati ya mitatu watakayocheza.

Kwa upande wa wanawake, JKT Stars iliyokuwa kinara kwenye hatua ya makundi kwa pointi 58 itachuana na Polisi iliyomaliza nafasi ya nane kwa pointi 47.

Michezo mingine itaendelea kesho kwa Don Bosco Troncatti dhidi UDSM Outsiders na Pazi Queens dhidi ya Vijana Queens.

Jumla ya timu nane kwa wanaume na nyingine nane kwa wanawake zitachuana na kupatikana nne kwa ajili ya kutinga hatua ya nusu fainali.