Daraja la Kiloka kujengwa

MOROGORO; Serikali imeshaidhininisha kiasi cha Sh Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kiloka linaounganisha Kijiji cha Kiloka na vijiji jirani, ambalo lilisombwa na maji ya mvua mapema mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miindombinu ya barabara na madaraja inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Morogoro.

Amesema serikali imetoa fedha hizo kurejesha mawasiliano katika vijiji hivyo, ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma za kijamii pamoja na zile za kiuchumi.

“Serikali imejikita kwenye ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua za El Nino,hivyo fedha hizi zitaenda kurejesha mawasiliano kwa kujenga daraja hili la Kiloka na vijiji vya jirani,” amesema.

Isome pia:https:https://habarileo.co.tz/bashungwa-aja-na-vipaumbele-9-ujenzi/

Mhandisi Mativila ameitaka TARURA kuendelea kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo, ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama ilivyokuwa awali.

Naye, Meneja wa TARURA Wilaya ya Morogoro, Mhandisi Mohamed Muanda ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha hizo, ambazo zitarejesha mawasilino ya vijiji vya jirani kupitia daraja la Kiloka.

Amesema fedha hizo zitajenga daraja hilo lenye urefu wa mita 12 na kuliwekea kingo za mto pamoja na ukarabati wa tuta la barabara.

Habari Zifananazo

Back to top button