Dart kukamilisha mfumo wa nauli kielektroniki

WAKALA ya Mabasi Yaendayo Haraka katika Mkoa wa Dar es Salaam (DART) imeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 3.03 kwa matumizi ya kawaida, ambazo miongoni mwa matumizi ni kukamilisha utengenezaji na usimikaji wa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji nauli.
Kwa mujibu wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 yaliyowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki, Sh bilioni 2.30 ni kwa ajili ya mishahara na Sh milioni 731.21 ni kwa matumizi mengineyo.
Kuhusu mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji nauli wa serikali (AFCS) unaosimamiwa na Dart, utafungamanishwa na mfumo wa kuongozea magari ikiwa ni sehemu ya maboresho endelevu ya huduma kwa wananchi waishio mijini, na pia kuondoa mianya ya upotevu wa mapato ya nauli kwenye mfumo.
Wakala pia itaendelea kuongeza mtandao wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuendelea na miundombinu ya awamu ya tatu itakayohusisha barabara zenye urefu wa kilometa 20.6 za Nyerere (Gongolamboto – Posta kupitia Sokoine), Uhuru (Buguruni – Kariakoo Terminal kupitia Mtaa wa Shaurimoyo na Lindi) na Shaurimoyo (Nyerere – Lindi).
Itakamilisha taratibu za ununuzi wa mtoa huduma za mabasi ya awamu ya kwanza na ya pili; kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa miundombinu ya mradi. Fedha hizo pia zinalenga kuboresha usafi wa mazingira katika mtandao wa wakala na kudumisha usalama kwa kuimarisha ulinzi katika mtandao wa Dart.
Wakala itaendelea na taratibu za kubadilisha mfumo wa uendeshaji na ulipaji wa watoa huduma kutoka kupokea tozo kupitia katika mfumo wa Dart na kuanza kutumia utaratibu wa malipo ya umbali wa mabasi yatakayokuwa yanatembea.
Katika hatua nyingine, Shirika la Masoko la Kariakoo limeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 1.68 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo sehemu zitaendelea na ujenzi wa soko jipya, ukarabati wa lililoungua linalotarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu. Kati ya kiasi hicho, Sh milioni 747.54 ni kwa ajili ya mishahara na Sh milioni 938.44 ni matumizi mengineyo.