Matumaini mapya kwa watu wenye VVU

MAREKANI : DAWA mpya ya kuzuia maambukizi ya VVU, iitwayo Lenacapavir, inatarajiwa kupatikana kwa gharama nafuu katika zaidi ya nchi 100 zenye kipato cha chini na cha kati ifikapo mwaka 2027. Hatua hiyo inatazamiwa kuwasaidia mamilioni ya watu wanaoishi na VVU na kuleta matumaini mapya ya kupunguza athari za janga la UKIMWI duniani.
Kwa sasa dawa hiyo inatarajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu kwa gharama ya Dola za Marekani 28,000 (takribani Sh milioni 70) kwa kila mtu kwa mwaka. Hata hivyo, wadau wamekubaliana bei hiyo ipungue hadi Dola 40 pekee, sawa na asilimia 0.1 ya gharama ya awali, ili kuhakikisha watu katika nchi zinazoendelea wanapata tiba hiyo.
Wanasayansi wanasema Lenacapavir hutolewa kwa njia ya sindano na hufanya kazi kwa kuzuia virusi vya VVU visijizalishe ndani ya seli za binadamu. Makubaliano hayo ya kihistoria yalitangazwa Jumatano, yakihusisha Wakfu wa Clinton, Gates Foundation na taasisi mbalimbali zikiwemo Wits RHI ya Afrika Kusini.
Mpango huo unasimamiwa na Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ambaye alishirikiana na makampuni ya dawa kuhakikisha dawa hiyo inawafikia watu wengi kwa gharama nafuu. Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mwendelezo wa jitihada za kimataifa za kuhakikisha dawa za kupunguza makali ya virusi zinapatikana kwa usawa katika nchi zote. SOMA: Maambukizi ya Ukimwi kuongezeka mara sita 2029