Unajua chakula ni salama kikikaa siku tatu tu kwenye jokofu?

DAR ES SALAAM: KUHIFADHI chakula kwenye jokofu ni njia bora ya kukilinda dhidi ya kuharibika na magonjwa yanayosababishwa na bakteria. Hata hivyo, usalama wa chakula haupatikani tu kwa kukiweka kwenye baridi, bali pia kwa muda unaokaa humo.

Wataalamu wa afya wanasema chakula kinachohifadhiwa kwenye jokofu kina muda maalumu wa kukaa kabla ya kuanza kupoteza ubora na usalama wake kwa matumizi ya binadamu.

Kwa ujumla, chakula kilichopikwa kinashauriwa kisikae zaidi ya siku tatu hadi nne kwenye jokofu lenye joto la chini ya nyuzi joto nne za sentigredi. Vyakula kama wali, nyama, samaki, kuku na maharage vilivyopikwa vinapaswa kuliwa ndani ya kipindi hicho, kwani baada ya hapo bakteria wanaweza kuanza kuzaliana hata kwenye baridi.

Vyakula vilivyobaki kutoka mlo wa awali vinapaswa kuwekwa kwenye vyombo safi vyenye vifuniko na kuingizwa kwenye jokofu muda mfupi baada ya kupoa, si zaidi ya saa mbili baada ya kupikwa. Kwa upande wa nyama mbichi, muda wa kuhifadhi unategemea aina yake.

Nyama ya ng’ombe na ya mbuzi inaweza kukaa siku tatu hadi tano kwenye sehemu ya baridi, ilhali nyama ya kuku au samaki inapaswa kutumika ndani ya siku mbili. Iwapo chakula kimehifadhiwa kwenye sehemu ya kufungia (friza) yenye joto la nyuzi joto 18 chini ya sifuri, kinaweza kudumu kwa miezi kadhaa, lakini ladha na virutubisho vinaweza kupungua kwa muda mrefu.

Ni muhimu pia kutokuruhusu chakula kilichohifadhiwa kuganda na kuyeyuka mara kwa mara, kwani mabadiliko hayo ya joto yanaongeza uwezekano wa bakteria kuongezeka.

Chakula kinachotolewa kwenye freezer kinapaswa kuyeyushwa polepole ndani ya jokofu, si kwa joto la kawaida, ili kudhibiti ukuaji wa vijidudu. Kwa vyakula vyenye maziwa kama maziwa mgando, jibini au siagi, muda wa kuhifadhi ni kati ya siku tano hadi 10 kulingana na aina yake, huku mayai yakishauriwa yasikae zaidi ya wiki tatu.

Matunda na mboga mbichi kwa upande mwingine hufaa zaidi ndani ya siku tano hadi saba, hasa yakihifadhiwa kwenye mifuko yenye hewa kidogo ili yasinyauke. Kwa hiyo, usalama wa chakula kwenye jokofu unategemea nidhamu ya kuhifadhi, muda wa matumizi na udhibiti wa joto.

Hata kama chakula kinaonekana kizuri au hakijanuka vibaya, hakikisha unazingatia muda uliopendekezwa. Kwa kufanya hivyo, unalinda afya yako na ya familia dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na vyakula vilivyoharibika kimyakimya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button