Dawa za kulevya milioni 2.3 zakamatwa 2024

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kwa mwaka 2024 limefanikiwa kukamata Dawa za kulevya  kilogramu 2, 327,983.66.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akieleza mafanikio waliyoyapata kwa kipindi cha mwaka 2024, Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema katika operesheni zilizofanyika mwishoni mwa mwaka 2024, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola zilikamatwa kilogramu 673.2 za methamphetamine na heroin.

“Kati ya dawa hizo, kilogramu 448.3 zilizowahusisha raia nane (8) wa Pakistani zilikamatwa Bahari ya Hindi zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini Pakistani kwa namba B.F.D 16548. Aidha, kilogramu 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam,” amesema Kamshina Lyimo.

Advertisement

Kamshina Lyimo amesema Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha inaikinga jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

“Kwa mwaka 2024, takribani watu milioni 28 walipewa elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya kupitia nyanja mbalimbali za uelimishaji, zikiwemo vyombo vya habari, semina na warsha, matamasha, mikusanyiko mbalimbali, na matukio ya kitaifa”.

“kwa Mwaka 2025 DCEA itaimarisha udhibiti wa dawa za kulevya nchini kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia za kisasa kufuatilia mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, utoaji wa elimu kwa umma ili kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na kujiepusha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya na kuendelea kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya kupitia programu za tiba na urekebishaji kupitia vituo vya tiba kwa waathirika vilivyopo nchini” amesema Kamshina Lyimo.

Mamlaka inawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga simu bure kupitia namba 119.