DC amaliza mgogoro wa ardhi Kigoma Ujiji

MKUU wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali amemaliza mgogoro wa ardhi katika Kata ya Bangwe Manispaa ya Kigoma Ujiji uliosababisha kusimamishwa kwa mradi wa maji kwa kile kinachoelezwa mradi huo umejengwa kwenye kiwanja cha mwekezaji bila makubaliano.

Katika mkutano huo Mkuu huyo wa wilaya aliendesha kikao baina ya wananchi na muwekezaji wa Kigoma Hilltop, Mohsin Abdallah Sheni, ambaye aliandika barua mamlaka ya maji safi na maji taka Kigoma Ujiji akitoa notisi ya siku 90 ya kuishtaki mamlaka hiyo kuingia na kujenga mradi kwenye eneo lake bila taarifa.

Awali Diwani wa Kata ya Bangwe, Hamisi Betese alimwambia Mkuu wa wilaya kuwa eneo linalolalamikiwa kwenye mradi na maeneo ya kuzunguka mradi  huo ni viwanja vya wananchi, ambao wamekuwepo hapo kwa muda mrefu na ndiyo walitoa eneo kwa mamlaka hiyo kujenga mradi huo.

Mkuu wa wilaya Kigoma Salum Kali (kushoto) na Mkurugenzi wa Hilltop Hotel, Mohsin Abdallah Sheni, wakipitia ramani ya eneo la Bangwe kuangalia eneo lenye mgogoro baina ya mwekezaji huyo na wananchi. (Picha zote na Fadhili Abdallah)

Betese alisema kuwa wameshangwaza kuona wakati tayari wamepandisha matanki ya kuhifadhi maji juu ili yaanze kujengwa baada ya serikali kupitia wizara ya ya maji kutoa  sh milioni 247 ya mradi huo na kubainisha kuwa jambo hilo linakwamisha juhudi za serikali za kupeleka huduma kwa wananchi.

Baada ya maelezo marefu ya viongozi wa kata na wananchi wa kata hiyo ya Bangwe, Kamishna wa Ardhi Mkoa Kigoma,Chadiel Mrutu, alitoa ramani ya eneo lote linalolalamikiwa na kueleza kuwa Kigoma Hilltop Hotel, ndiyo mmiliki halali wa kiwanja namba 13 hadi 15, vyenye mgogoro ambavyo alimilikishwa mwaka 1996 akiwa na hati ya miaka 99.

Kamishna huyo wa ardhi Mkoa Kigoma alisema kuwa mradi huo wa maji umejengwa ndani ya kiwanja cha Kigoma Hilltop Hotel, ambayo ipo chini ya uendeshaji wa mwekezaji, Mohsin Abdallah hivyo mradi huo na viwanja vingine 40 vimeingia eneo hilo isivyo halali.

Sambamba na hilo alisema kuwa pia viwanja namba 16 hadi 20 navyo ni mali ya Kigoma hilltop Hotel Ltd, vikiwa na ofa ya tangu mwaka 1996 na jumla ya viwanja vyote vina ukubwa wa hekta 38.7 sawa na hekari 96.75 na vyote amevipata kupitia taratibu halali za kiserikali.

Kufuatia maelezo hayo Mkuu wa wilaya Kigoma alimwomba mwekezaji huyo ambaye aliitwa kuja kwenye mkutano huo na Mkuu wa wilaya aeleze anavyoujua mgogoro huo na tuhuma za kusimamisha mradi na kutaka kuwaondoa watu kwenye eneo hilo.

Akieleza kuhusu notisi ya siku 90 ya kusimamisha mradi huo wa maji Sheni alisema kuwa aliwapigia uongozi wa mamlaka ya maji na diwani kutaka wampe barua ya kuomba kuptisha barabara kwenye eneo la mradi, ili kupitisha mabomba lakini hawakufanya hivyo.

Aliongeza mara kadhaa aliendelea kuwapigia simu lakini hawakutekeleza agizo la kuwataka waandike barua kuomba kupitisha barabara hiyo na badala yake walisikika wakisema kuwa hilo siyo eneo la mwekezaji huyo na hawana sababu ya kuandika barua hiyo.

Diwani wa kata ya Bangwe Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hamisi Betese.

Akihitimisha mjadala kuhusu mradi huo, Sheni  alisema kuwa pamoja na yote yalitokea hakuwa na nia ya kuzuia kutekelezwa kwa mradi, lakini alitaka taratibu za yeye kutoa eneo zifuatwe na kwamba ameridhia mradi wa maji kuendelea kutekelezwa.

Wakati hatima ya mradi ikitatuliwa bado Mkuu wa wilaya alisema kuwa kuna tatizo la wananchi kuingia eneo la mwekezaji na kujenga makazi, hivyo utafanyika ukaguzi na uhakiki wa mipaka na baada ya hapo mgogoro huo utatolewa tamko.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Diwani wa kata ya Bangwe, Hamisi Betese akiongoza viongozi wa mitaa mitatu katika kata hiyo aliitisha kikao cha hadhara cha wananchi kueleza mgogoro huo na kuwataka wananchi hao kwenda kwenye maeneo hayo na kuchukua kila mtu na eneo lake, kwani mwekezaji amechukua maeneo makubwa, huku wananchi wakiwa hawana maeneo yakiwemo ya huduma za kijamii.

Habari Zifananazo

Back to top button