DC ataka utaratibu migogoro ya ardhi

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mshamu Munde amewataka wananchi wenye migogoro ya ardhi kuanzia ngazi ya chini kuliko kukimbilia ofi sini kwake.

Munde aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO na kueleza kuwa kumeibuka tabia ya wananchi kukimbilia ofisi ya Mkurugenzi wakati migogoro hiyo inaweza kutatuliwa na wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji na kata.

“Ofisi ya Mkurugenzi ina mambo mengi ya kufanya ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo natoa rai mwananchi yeyote anayekuja ofisini kwangu kwa ajili ya migogoro ya ardhi ahakikishe ana barua kutoka kwa mtendaji wa kijiji au kata inayoonesha kwamba suala lake limekosa ufumbuzi kwa ngazi ya kijiji,” alisema.

Aidha, Munde alisema kukimbilia kwa Mkurugenzi kwa kigezo kuwa wenyeviti na watendaji ni chanzo cha migogoro haitoshi kujiridhisha kwani viongozi hao wapo kwa mujibu wa sheria na wanalipwa kwa kutimiza wajibu wao.

Vilevile Munde alisema kuwa kwa sasa kumeibuka utapeli ambapo baadhi ya madalali wanakuwa na hati feki halafu wanafungua kesi kwenye mabaraza ya ardhi mmoja wao anashinda kesi, akishinda kesi anauza ardhi na kisha wanagawana fedha na yule aliyeshinda huku mwenye ardhi kihalali hajui kinachoendelea.

“Ofisi yangu kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) tayari ina taarifa hizo na zinafanyiwa uchunguzi kwa kina na utakapokamilika watafikishwa mahakamani,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button