DC, halmashauri wamshukia mweka hazina Iringa Vijijini

MWENZA Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Jwani Maria Yengi, amenyoshewa kidole na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Benito Kayugwa, akilalamikiwa kuwa na utendaji usioridhisha na kukosekana kwa ushirikiano na watumishi wenzake.

Katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika leo mjini Iringa, Mkuu wa Wilaya alizungumzia changamoto za utendaji za mweka hazina huyo na kuwepo kwa mianya ya upotevu wa mapato ndani ya halmashauri.

James alisisitiza kuwa ni lazima mweka hazina huyo ajitafakari na kuchukua hatua madhubuti za kurekebisha dosari zilizopo ofisini mwake ili kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha uadilifu katika ukusanyaji wa mapato.

Advertisement

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Benito Kayugwa, ameeleza kutoridhishwa kwake na uwajibikaji wa mweka hazina huyo, akifafanua kuwa Yengi ni mtumishi pekee ambaye amekuwa hapokea simu zake za kikazi, hivyo kusababisha changamoto za mawasiliano na kurudisha nyuma utekelezaji wa majukumu ya madiwani.

“Nakuomba Mkurugenzi wa Halmashauri utusaidie kushughulikia changamoto hii. Ni muhimu mtumishi huyu afahamu kuwa jukumu lake linahitaji ushirikiano ili kufanikisha mipango ya halmashauri yetu,” amesema Kayugwa.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ametoa agizo kali kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo, akiwataka kuacha tabia ya kuwakaribisha wageni rasmi kwenye mahafali na shughuli za shule bila kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri.

James amesema kuwa baadhi ya wageni wamekuwa wakitumia majukwaa ya mahafali kwa maslahi binafsi, hususan kwa masuala ya kisiasa, badala ya kuzingatia lengo kuu la shughuli hizo.

“Ni vyema wageni waalikwa wafanye kazi wanayotakiwa kufanya, sio kugeuza majukwaa haya kuwa sehemu ya shughuli zao binafsi,” amesema James.

Pia, Mkuu wa Wilaya amewataka wakuu wa shule kuachana na utaratibu wa kufanya harambee wakati wa mahafali, akisisitiza kuwa wazazi wanahudhuria mahafali kwa lengo la kusherehekea mafanikio ya watoto wao, na siyo kwa michango ya harambee.

Mkurugenzi wa Halmashauri, Robert Masunya, ameongeza kuwa itifaki inataka taarifa za mialiko yote ya wageni rasmi zipitie kwake ili kuhakikisha mgeni anayealikwa anafaa na yupo kwenye malengo sahihi.

“Tuna watu wanaalikwa kwenye mahafali hadi mawaziri au watu kutoka nje ya mkoa bila Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya, wala Mkuu wa Mkoa kufahamu. Huu sio utaratibu unaokubalika,” amesema Masunya, akisisitiza umuhimu wa kufuata msingi sahihi ili kupata wageni rasmi wenye tija kwa shughuli husika.