DC Lindi aipongeza YST hamasa masomo ya sayansi

LINDI; SERIKALI ya Mkoa wa Lindi imesema inafurahishwa na kuunga mkono Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) kwa kuandaa maonesho ya kazi za bunifu za sayansi na teknolojia zinazofanywa na wanafunzi katika mkoa huo.

Akizungumza katika maonesho ya nne ya kazi bunifu za sayansi na teknolojia Mkoa wa Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amesema hatua hiyo imekuwa chachu katika kuunga mkono jitihada za serikali  kuendeleza masomo ya sayansi nchini.

Amesema  maonesho hayo yamekuwa chachu katika kuibua na kuhamasisha wanafunzi wengi kuvutiwa na masomo ya sayansi.

“Tunashukuru sana Taasisi ya Young Scientists Tanzania kwa kuratibu na kuandaa maonesho ya kazi bunifu za sayansi na teknolojia kwenye mkoa wetu, hatua hii imekuwa chachu katika kuhamasisha wanafunzi wengi kupenda masomo ya sayansi,” amesema.

Maonesho hayo yameandaliwa kimkoa kuchagua kazi bora za bunifu za sayansi na teknolojia kutoka kwa wanafunzi wa shule za secondari Mkoa Lindi na baadae kushindanishwa katika maonesho ya kitaifa.

Akizungumzia kazi bunifu za sayansi na teknolojia zilizofanywa na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Mkoa wa Lindi, Mwanziva amesema serikali ya Mkoa itachukua kazi hizo na kuzifanyia kazi ili kuziongezea thamani.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button