MKUU wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Salumu Kalli amewataka wanamichezo wilayani humo kumuunga mkono Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Longido,Dk Steven Kiruswa katika azma yake ya kuibua vipaji katika michezo kwani michezo ni ajira na burudani.
Kalli amesema hayo baada ya kukagua timu mbili za Viwawa Fc na Namanga Veterani zilizokutana katika mchezo wa fainali wa Kombe la Kiruswa Jimbo Cup mashindano yaliyoasisiwa na mbunge kwa zaidi ya miaka minne yenye lengo la kuibua vipaji vya soka.
Amesema soka ni ajira kubwa kwa sasa duniani na vijana wengi wanamiliki miradi mikubwa na midogo kutokana na soka hivyo aliwaomba vijana wanaoshiriki Kiruswa Jimbo Cup kutumia mashindano hayo kusonga mbele.
Kikosi cha timu ya Namanga Veterani kilichotwaa ubingwa
Mkuu huyo wa wilaya amesema kutokana na hali hiyo Mbunge wa Jimbo la Longido anapaswa kuungwa mkono katika jitihada zake za kuinua vipaji Longido na kumwacha mwenye ni kumkosea hivyo juhudi za ziada zinahitajika kuongeza nguvu katika mashindano hayo ikiwa ni pamoja kuongeza zawadi kwa washindi wa Kiruswa Jimbo Cup.
Akizungumzia uwanja Mkuu wa Wilaya aliwataka viongozi wa michezo Halmashauri kutafuta eneo ili kujengwe uwanja mzuri wenye tija kwa ajili ya soka kuliko uwanja wa Polisi Longido ambao umejaa vipara na hauna hadhi kisoka.
‘’Tunataka uwanja wa Kisasa Longido ili wana soka waweze kucheza soka safi katika uwanja huo hivyo idara ya michezo Longido inapaswa kuwajibika kwa hilo,” amesema Kalli.
Mgeni rasmi Mwamvita Okeng’o akikabidhi zawadi akiwa na mke wa Naibu Waziri wa Madini Na Mbunge wa Longido,Dk Steven Kiruswa Kiruswa
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Wilaya ya Longido, Obei Mollel amesema mashindano ya Kiruswa Jimbo Cup yalianza rasmi septemba 24 mwaka huu kwa kushirikisha timu 50 za Jimbo hilo na washiriki wote walipewa zawadi ya seti ya jezi na mpira mmoja mbali ya zawadi ya mshindi wa kwanza hadi wa tatu wa mashindano hayo.
Mollel alisema mchezaji chipukizi wa mashindano hayo alipewa Hiral Kitila mwenye umri wa miaka 18 na amepewa nafasi ya kucheza mashindano ya Kimataifa ya Future Academ yatakayofanyika desemba mwaka huu jijini Arusha ,mfungaji bora alikuwa Emmanuael Gabriel, golikipa bora alikuwa Abubakar Abuu, timu ya Young Boys imepata zawadi ya timu yenye nidhamu.
Mkuu wa Wilaya ya Longido,Salumu Hassan Kalli akikagua timu na kuongea kabla ya mchezo wa fainali kupigwa kati ya bingwa mtetezi Viwawa FC ambaye amevuliwa naNamanga Veterani mabingwa wapya.
Ofisa Michezo Mkoa wa Arusha,Mwamvita Okeng’o alikabidhi zawadi kwa bingwa wa Kiruswa Jimbo Cup timu ya Namanga veteran baada ya ushindi wa Goli 1-0 dhidi ya Viwawa Fc goli lililofungwa na Ismail Azizi Kada katika mchezo mkali wa fainali na bingwa kujinyakulia Sh milioni 1,seti ya jezi na medali.
Okeng’o alikabidhi zawadi ya mshindi wa pili kwa timu ya Viwawa Fc Sh 500,000,medali na seti ya jezi na Mshindi wa tatu ilikwenda kwa timu ya Irkaswa na kufanikiwa kupata Sh 300,000,medali na seti ya jezi.