Vijana washauriwa kuwekeza soko la hisa

ARUSHA: Vijana wameshauriwa kuwekeza katika soko la hisa ili kujenga uchumi kupitia uwekezaji wa kidijitali na kujikwamua kiuchumi huku wakijiandaa na maisha ya baadaye.
Wito huo umetolewa leo jijini Arusha na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa benki hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 15 na 16 mwaka huu ukiwa na kauli mbiu“Vijana na Uwekezaji katika Hisa”.

Profesa Mori amesema mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Musa Omari ambapo mwaka huu benki hiyo imependekeza gawio la Sh 90 kwa kila hisa, ikiwa ni ongezeko kutoka sh, 65 zilizotolewa awali, hatua ambayo aliieleza kuwa ni mafanikio makubwa kwa wanahisa na bodi ya benki hiyo.
“Ni wakati wa vijana kununua hisa na kuwa wawekezaji ili waweze kutumia ubunifu wa kidijitali kuonyesha vipaji vyao na kujikwamua kiuchumi,” alisema Profesa Mori.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela, amewashukuru wadau, wateja na bodi ya wakurugenzi kwa mchango wao katika kufanikisha malengo ya benki hiyo.
Amesema bodi imeendelea kutoa ushauri na maelekezo yenye tija yaliyochangia maboresho makubwa kwa wanahisa pamoja na kuweka mipango ya maendeleo ya sasa na ya baadaye.



