DC Mgomi aridhishwa utekelezaji miradi Ileje

SONGWE: MKUU wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Farida Mgomi, amefanya ziara ya kukagua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.
Akiwa katika ziara hiyo, DC Mgomi ameridhishwa na namna miradi hiyo inavyotekelezwa kwa kuzingatia weledi na viwango vya ubora, na hivyo kuwapongeza wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kwa juhudi zao katika kusimamia vyema miradi hiyo ili kufanikisha azma ya serikali ya kuinua ustawi wa wananchi.

Miongoni mwa miradi aliyotembelea ni mradi wa upanuzi wa Shule ya Sekondari Izuba, iliyopo Kata ya Isongole, unaohusisha ujenzi wa mabweni mawili, nyumba ya walimu (2 in 1), vyumba vinne vya madarasa pamoja na matundu 10 ya vyoo.
Miradi hiyo kwa pamoja imegharimu jumla ya Sh milioni 480 na ipo katika hatua za mwisho kukamilika.

Mabweni na nyumba ya walimu vipo hatua ya umaliziaji, huku madarasa na vyoo vikiwa tayari vimekamilika.

Aidha, Mgomi alikagua pia ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ileje pamoja na ukamilishaji wa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya wilaya.

Miradi huo umepokea jumla ya Sh milioni 350 kutoka Serikali Kuu ili kukamilika.
Katika ziara hiyo, DC Mgomi alimewataka wasimamizi wa miradi kuhakikisha wanakamilisha kazi hizo kwa wakati ili ziweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi, sambamba na kutekeleza kwa vitendo azma ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha maisha ya Watanzania.





