DC Mtwara ataka mikakati matokeo sekondari

MKUU wa Wilaya ya Mtwara ya Mtwara Abdallah Mwaipaya amewataka walimu kutoka shule mbalimbali za sekondari katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara kuhakikisha wanazingatia mikakati yote waliyojiwekea ili kuendelea kuleta matokeo mazuri kwa watoto wao.

Akizungumza wakati wa ghafla fupi ya kuwapongeza walimu hao kuhusu kazi mzuri waliyoifanya kwa kuleta matokeo mazuri ya kidato cha nne mwaka 2024 katika manispaa hiyo, mkuu huyo wa wilaya amesema matokeo ya wanafunzi wao wanayoyafurahia kwa sasa ni alama na uthibitisho tosha wa kazi mzuri na iliyotukuka kutoka kwa walimu hao.

Ghafla hiyo imeandaliwa na Manispaa ya Mtwara Mikindani lengo likiwa ni pamoja na kutoa pongezi na hamasa lakini pia kuendelea kutambua mchango mkubwa unaofanywa na walimu kwa kuendelea kulea matokeo mazuri ya wanafunzi kwenye manispaa hiyo.

Pongezi hizo zimeambatana na utoaji wa vyeti na fedha kiasi cha Sh milioni 23.5 kwa walimu na watendaji kwa baadhi ya shule hizo ikiwemo sekondari ya Shangani pamoja na Mtwara Ufundi kutoakana na kufanya vizuri zaidi kwenye matokeo hayo.

Aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kuboresha miundombinu ya shule inayopolekea walimu hao wakawa na mazingira mazuri ya kufundisha.

‘’Leo hii tunashuhudia madarasa vioo vya aluminiamu, tailizi mapaka feni, ni mazingira mazuri sana ambayo mheshimiwa Rais ameweza kuyaweka na kuleta fedha nyingi kwenye sekta yetu ya elimu,’’amesema Mwaipaya

Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mwalimu Hassan Nyange amesema kipaumbele cha kwanza kwake ni elimu na utaratibu huo utakuwa endelevu kadri ambavyo Mwenyezi Mungu atavyowapatia nafasi ili waipe heshima sekta hiyo ya elimu pamoja na walimu kwa ujumla.

Amesema walimu hao ni lazima wajivunie ualimu wao huku akiwasisitiza kuwa wabunifu na wasimamizi wa elimu ambapo uongozi wa manispaa hiyo uko makini na usimamizi wa masuala yote yanayohusika na elimu.

Baadhi ya walimu hao akiwemo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi, Riyadhi Abubakar amesema watahakikisha wanaendelea kuleta matokeo mazuri kwasababu wanapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa uongozi wa manispaa hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button