DC Nyamagana: Bidhaa zenu zikidhi viwango vya TBS

MWANZA; Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Jubilate Lauwo, amewataka wafanyabiashara kutumia kwa usahihi fursa ya uwepo wa Kliniki ya Viwango (Viwango Clinic), iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.

Ametoa kauli hiyo jijini Mwanza leo Oktoba 21, 2026 wakati akifungua kliniki hiyo na kuwataka wafanyabiashara wa bidhaa za chakula na vipodozi kutumia fursa hiyo kusajili bidhaa zao, hatua itakayosaidia pia kuongeza imani kwa wateja wao.

“Wafanyabiashara mnapaswa kuhakikisha bidhaa mnazouza ni salama na zinakidhi viwango vinavyotakiwa na TBS, hivyo mna wajibu wa kuzingatia taratibu za biashara zenu kwa kuhakikisha mnasajiliwa,” amesema Lauwo.

Amesema Viwango Clinic ni fursa kwa wafanyabiashara wa bidhaa za chakula na vipodozi jijini Mwanza kupata elimu na huduma ya usajili karibu yao, huku pia wananchi wakipata elimu itakayowasaidia kuepuka matumizi ya bidhaa zisizokidhi viwango vya TBS.

“Kwa mujibu wa mwongozo wa TBS, wafanyabiashara wa chakula na vipodozi wanapaswa kuzingatia taratibu za usajili wa bidhaa, maeneo ya biashara zao kama vile maghala, maduka na migahawa,” amesisitiza Lauwo kwenye ufunguzi huo uliohudhuriwa pia na viongozi, wananchi na wafanyabiashara mbalimbali.

Naye Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, Happy Brown amesema Viwango Clinic inayofanyika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza itadumu kwa siku tano ilianza Jumatatu Oktoba 19, 2026 na itamalizika Ijumaa Oktoba 23, 2026 ambapo lengo ni kusogeza elimu na huduma karibu na wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button