DCEA yakamata skanka kilogramu 1,815

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DCEA) imekamata kilogramu 1,815 za dawa za kulevya aina ya skanka katika operesheni iliyofanyika tarehe 28 Agosti, 2024 hadi tarehe 02 Septemba, 2024 katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo watuhumiwa watano  wamekamatwa.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Kamishna wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema watuhumiwa waliokamatwa ni Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Felista Henry Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguluni Mbezi wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya.

“Watuhumiwa wengine ni Athumani Koja Mohamed (58) mfanyabiashara, na mkazi wa Tanga, Omary Chande Mohamed (32) dereva bajaji na mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam na Juma Abdallah Chapa (36) mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam.  Aidha, katika operesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa”

“Richard Mwanri ni mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa siku za hivi karibuni, dawa za kulevya aina ya skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara nchini” Amesema Lyimo.

Skanka ni aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, figo, na ini. Matumizi ya skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Dunia iliyotolewa Vienna nchini Austria tarehe 26 Juni, 2024, maeneo yaliyohalalisha matumizi ya bangi, uzalishaji wa bidhaa za bangi zenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC uliongezeka.

SOMA :DCEA yakamata dawa za kulevya kilo 3,182

Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuwa, katika nchi hizo, kumekuwa na ongezeko la watu wanaohitaji tiba kutokana na matumizi ya bangi sambamba na kuongezeka kwa watu wenye matatizo ya akili na waliojaribu kujiua.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawasihi wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara hii haramu na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara wala matumizi ya dawa za kulevya.

SOMA : DCEA YAKAMATA KILO 1,815 ZA SKANKA, WATUHUMIWA WATANO WAKAMATWA

Habari Zifananazo

Back to top button