MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Grace Quintine amesema kinachopelekea watoto wa kike kutopenda kusoma masomo ya sayansi ni kutokana na kukatishwa tamaa na watu wanaowazunguka.
DED Quintine amesema hayo wakati akifungua semina ya siku mbili ya kuhamasisha mtoto wa kike kupenda na kusoma masomo ya sayansi wilayani Urambo.
Kampeni hiyo inayohusisha Semina pamoja na ufuatiliaji wa matokeo imefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Kitaifa ya Wasichana ya Margareth Sitta na kuhusisha walimu wakuu wa shule za sekondari 17, walimu wa masomo ya sayansi, viongozi wa serikali za vijiji na vitongoji pamoja, viongozi wa dini pamoja na wawakilishi wa wazazi.
Katika ufunguzi wa semina hiyo Mkurugenzi Quintine amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amejikita kuweka usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali, lakini pasipo na watoto wa kike wengi wenye elimu itakuwa ngumu kupata wanawake watakaofaa ngazi za juu.
Aidha, Quintine amesema kuwa mtoto wa kike ana upeo mkubwa wa kiakili ambapo anaweza kusoma masomo hayo na kufaulu. Amejitolea mfano kuwa hata yeye alifaulu masomo hayo kwa kuyasoma kwa miezi kadhaa alipokuwa sekondari.
Hata hivyo amesema jamii inapaswa kuepukana na mila kandamizi kwa mtoto wa kike kwani watoto wote wa kike na wakiume wana haki sawa.