‘Demokrasia haijengwi kwa kuvuruga amani’

“Demokrasia ni gharama, lakini amani, usalama, ulinzi na utulivu wa nchi yetu ni gharama sana.”
Anasema Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Esther Matiko anapozungumzia hali ya uchokonozi inayoendelea katika mitandao ya kijamii.

Hivi karibuni Serikali ya Tanzania iliwakamata wanaharakati wa Kenya waliokuwa wakiingia nchini kwa madai ya kutaka kuhudhuria kesi ya Mwenyikiti wa chama hicho, Tundu Lisu anayekabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo, Lissu anadaiwa kutamka na kuchapisha maneno yanayodaiwa kuwa na nia ya kuchochea vurugu na kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Katika hati hiyo ambayo gazeti la HabariLEO lilisikia kusomwa kwake mahakamani, inadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, Lissu alinukuliwa akisema: “… Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli… Kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hiyo ndiyo namna ya kupata mabadiliko… Kwa hiyo tunaenda kukinukisha… sanasana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kweli kweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Katika kauli hiyo na nyinginezo ambazo, Lisu aliwahi kutamka kwenye mikutano yake, anadai anapambania demokrasia na haki za Watanzania kwa kutaka mabadiliko ya katiba yaliyomfanya aibuke na kaulimbiu ya ‘No Reforms, No Election’ yaani bila mabadiliko, hakuna uchaguzi.
Serikali katika kesi hiyo inadai kauli hiyo inaashiria nia ya wazi ya kuchochea wananchi kuzuia uchaguzi na kuvuruga utulivu wa kitaifa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Kesi ya Lisu inawaibua wanaharakati na wanasiasa wa Kenya ambao nao wanaamua kuungana na Lisu na kufunga safari hadi Tanzania kuhudhuria kesi hiyo.
Miongoni mwa wanaharakati hao ni Martha Karua, Jaji mstaafu Willy Mutunga, Boniface Mwangi wa Kenya na Agatha Atuhaire wa Uganda. Kukamatwa kwa wanaharakati hao kunaibua ukosefu wa nidhamu dhidi ya viongozi wa nchi. Kwa kiasi kikubwa, watumiaji wa mitandao hiyo wanaokosa nidhamu ni Wakenya.
Matiko anasema hii si mara ya kwanza viongozi wa upinzani kuwekwa ndani. Hata hivyo, anabaki na maswali kwamba, kuna ajenda gani chini ya kapeti inayotoa msukumo kwa haya yanayoendelea kwa sasa kuhusiana na kesi ya Lisu na ushiriki wa wanaharakati wa Kenya.
“Huko nyuma hatukuwahi kuona haya mambo yakitokea, kwa nini yatokee sasa? Kuna jambo linafichwa!” “Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwahi kukaa ndani kwa muda mrefu, lakini hatukuona aina hii ya dharau kwa viongozi,” anasema Matiko.
Anasema Rais Samia alipoingia madarakani aliona umuhimu wa demokrasia kwa siasa za Tanzania kiasi cha kuanzisha Falsafa ya 4R iliyokuwa na lengo la kuimarisha demokrasia na akaruhusu mikutano ya vyama vya siasa. Awali, mikutano hiyo ilikuwa imefungiwa na hawakuweza kufanya hata mikutano ya kamati kuu za vyama.
“Mheshimiwa Spika, Mama (Rais Samia) alikuja na 4R, tunajua kabisa mimi ni mpinzani huko nyuma tulikuwa hatuwezi kufanya hata vikao vya kamati kuu ya chama ndani ya jengo… “Tulikuwa hatuwezi kufanya mikutano ya hadhara, lakini Mama kupitia 4R yake, watu wanafanya mikutano ya hadhara na kunakuwa na uhuru wa kujieleza.”
Anasema hii si mara ya kwanza viongozi wa upinzani kukaa gerezani akitolea mfano wake na Mbowe walipokaa gerezani.
Anaongeza kuwa, wakati huo hayakufanyika mambo kama hayo yanayotokea wakati huu. “… Hatukuwahi kuona haya mambo yakitokea, kwa hiyo inabidi tukae kama nchi tujiulize kuna kitu gani chini ya kapeti?” “Kwa nini sasa hivi, kwa hiyo tusitumie hiyo nafasi ambayo Mama ametoa ya 4R zake kuharibu taifa letu,” anasema Matiko.
“Demokrasia ni gharama lakini amani, usalama, ulinzi na utulivu wa nchi yetu ni gharama sana, lazima tuangalie leo tuna hii amani tunaweza tukafanya kila tunachofanya,” anaongeza. Matiko anasema cha kusikitisha ni kuwa, hata baadhi ya Watanzania wanashiriki utovu huo wa nidhamu bila aibu. Ndipo anahoji zilipo mamlaka husika kutafuta mwarobaini wa jambo hilo.

Anazihimiza mamlaka za Kenya na Tanzania kushirikiana kukabiliana na utovu huo wa nidhamu mitandaoni unaolenga kuchafua viongozi na kuvuruga amani ya nchi. Kauli hiyo ya Matiko haitofautiani na mawazo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi anayesema demokrasia haijengwi kwa siasa za kuchafuana ndani wala nje ya chama.
Anasema demokrasia imara hujengwa kwa hoja zinazoamsha ari kwa wananchi na wasio wananchi kushiriki ajenda za maendeleo. Dk Nchimbi anawataka wana CCM kuachana na kampeni chafu hasa wale wanaowachafua wabunge walioko madarakani katika maeneo mbalimbali.
“Kumeibuka tabia ya wana CCM ambao wameanza kampeni chafu za kuchafua wenzao. “Wapo wanaochapisha hadi ‘T-shirts’ (fulana) ambazo zimeandikwa maneno ya kashfa kwa wale walioko madarakani. Hii si sawa,” anasema. Anaweka wazi kuwa, CCM haitokuwa tayari kupitisha wanachama wa aina hiyo kuwa wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu badala yake, majina yao yatakatwa.
Akizungumzia vyama kushiriki uchaguzi, Dk Nchimbi anasema ni suala la kidemokrasia mtu kutumia haki ya kuchagua au kuchaguliwa katika uchaguzi, lakini hakuma chama kitakacholazimishwa kushiriki uchaguzi. “Ni kosa kubwa sana kukilazimisha chama cha siasa kuingia kwenye uchaguzi,” anasema.
Nchimbi anawataka wana CCM kutolazimisha Chadema kushiriki uchaguzi kwa sababu wanachokifanya ni haki yao. Katika kuonesha kuwa hayuko tayari kuona falsafa ya 4R inakuwa mlango wa kuchochea vurugu na uasi wa kisiasa kwa kigezo cha kudai demokrasia, Rais Samia anasema hawezi kuacha nchi iingiliwe na yeyote atakaye.
Anavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kusimama katika nafasi yake na kushughulikia viashiria vyote vya uvunjifu wa amani na utulivu. Anazitaka mamlaka za ulinzi na usalama zinazonyooshewa vidole kutokaa kimya badala yake, zitoe majawabu na ufafanuzi wa yale yanayosemwa ili kuweka sawa amani na hali ya kisiasa nchini.
Kuhusu wanaharakati wanaoingia nchini kuhudhuria kesi ya Lisu, Rais Samia anasema hawezi kuruhusu waingie na kuivuruga amani ya nchi kwa kuwa moja ya majukumu aliyokabidhiwa ni kuilinda amani ya nchi.
“… Tumeanza kuona mwenendo wa wanaharakati ndani ya eneo letu hili kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku, sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku, tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, nchi iliyobaki haijaharibika, watu wako na amani, usalama na utulivu ni hapa kwetu,” anasema.
Rais Samia. Kiuhalisia hakuna nchi inayoweza kuimarisha demokrasia kwa kuvuruga amani kwa kuwa amani
ya nchi inapotoweka mara moja haiwezi kurejea.