Dereva wa basi awekwa chini ya ulinzi wodini

MOROGORO; POLISI mkoani Morogoro, imemuweka chini ya ulinzi akituhumiwa uzembe na kusababisha ajali, dereva wa basi la Kampuni ya Rungwe Express, Selemani Matimbwa (50), ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo.

Dereva Matimbwa amelazwa hospitali hiyo kutokana na kujeruhiwa katika ajali ya basi la Rungwe Express kugongana uso kwa uso na lori na kupoteza uhai wa abiria mmoja na kujeruhi wengine watano, akiwemo dereva huyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Alex Mkama amesema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 24, 2025 katika eneo Kijiji cha Mkata, Kata ya Msongozi , Wilaya ya Mvomero Barabara Kuu ya Morogoro- Iringa.

Amesema ajali hiyo imehusisha gari namba T.393 DFQ Yutong Basi la kKmpuni ya Rungwe Express ikitokea Dar es Salaam kwenda mkoani Mbeya kugongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T.925 DZW na tela namba T.425 EAD aina ya Scania lililobeba mzigo wa mbao likitokea Iringa kwenda Dar es Salaam.

Mkama amesema basi hilo lilikuwa linaendeshwa na Matimbwa ambaye ni mkazi wa Chamwino, Manispaa ya Morogoro na lori hilo likiendeshwa na Martin Kilwale (25) mkazi wa Mafinga, mkoani Iringa na hivyo kusabaisha kifo cha abiria mwanamke ambaye bado hajatambuliwa na majeruhi watano.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi lkutaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kusababisha kugongana uso kwa uso na Lori hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button