DG NEMC akutana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu) Dk Jim James Yonazi akutana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Immaculate Sware Semesi akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya NEMC leo Aprili 30 jijini Dodoma kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya kimazingira.
Aidha, changamoto kadhaa zinazoikabili nchi yetu zimejadiliwa ikiwa ni pamoja na uchafuzi na uharibifu wa mazingira, kupotea kwa bionuai, uwepo wa magugu maji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Ziwa Victoria.

Kufuatilia changamoto hizo Katibu Mkuu Dk Yonazi amesisitiza mashirikiano kati ya Wizara na Taasisi za Serikali katika kukabiliana na changamoto za hizo za kimazingira.
Aidha, Dk Yonazi amepongeza jitihada za NEMC katika kusimamia mazingira nchini, pia ametoa rai kwa taasisi za ndani kujengewa uwezo wa technolojia na vifaa mahususi vitakavyosaidia kutatua changamoto za kimazingira nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dk Semesi, ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jitihada zake za kuhakikisha maendeleo endelevu nchini yenye kuzingatia uhifadhi wa mazingira, akiahidi kwamba baraza litaendelea kutoa ushirikiano na kuwa tayari pale litakapohitajika.



