Dhahabu na BRICS: Njia mpya ya Tz kulinda uhuru wa kifedha

DAR ES SALAAM, Oktoba 2025 – Wakati mataifa makubwa duniani yakizidisha kanuni za kifedha na kuimarisha utawala wa Dola ya Marekani, Tanzania inakabiliwa na shinikizo jipya la kusawazisha kati ya uthabiti wa uchumi na uhuru wa kisera.
Wachumi wanatahadharisha kuwa mifumo ya kifedha inayoendeshwa na Magharibi kuanzia masharti ya IMF hadi sera mpya za kodi za kimataifa inaweza kupunguza nafasi ya Tanzania katika kuamua sera zake za kiuchumi.
Kwa kasi inayoongezeka, viongozi na wasomi nchini wanauliza iwapo Tanzania inapaswa kuelekeza juhudi zake kwenye akiba za dhahabu na mifumo ya kifedha inayoendeshwa na nchi za BRICS, ili kurejesha uhuru wa sera za fedha.
Kwa miongo kadhaa, Marekani na washirika wake wamejenga utawala wa kifedha duniani kuzunguka Dola ya Marekani. Takribani asilimia 60 ya akiba za fedha duniani na biashara za kimataifa bado zinatumia dola, hali inayowapa Washington na taasisi za Magharibi nguvu kubwa juu ya uchumi wa nchi zinazoendelea.
Kutegemea kwa Tanzania programu za IMF na Benki ya Dunia kunadhihirisha changamoto hiyo. Fedha za mikopo zenye jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.25 kupitia Extended Credit Facility (ECF) na Resilience and Sustainability Facility (RSF) zimeisaidia nchi kudumisha uthabiti wa uchumi na kuimarisha hali baada ya janga la COVID-19, lakini masharti yake ya kimfumo yanaathiri sera za kodi na ruzuku za mafuta.
“Mipango hii inatusaidia kudhibiti thamani ya shilingi na mfumuko wa bei, lakini pia huambatana na masharti yasiyoendana na uhalisia wetu wa ndani,” alisema Profesa Humphrey Moshi, mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Wakati kila uamuzi wa kifedha unategemea tathmini kutoka Washington au Brussels, uhuru wa taifa unakuwa suala la mazungumzo.”
Maafisa wengine wanakiri kwa faragha kuwa nafasi ya Tanzania katika kubadilisha sera za kifedha inapungua. Mipango ya IMF kwa kawaida huhitaji serikali kupunguza matumizi, kuongeza mapato ya ndani na kudhibiti fedha hatua zinazowavutia wawekezaji, lakini zinazochukuliwa kuwa kandamizi kwa sekta za ndani.
Shinikizo Jipya: Kodi ya kimataifa ya angalau asilimia 15
Serikali za Magharibi sasa zinasukuma utekelezaji wa kodi ya chini ya kimataifa ya angalau asilimia 15 kwa kampuni kubwa, kwa madai ya kuzuia ukwepaji kodi. Hata hivyo, wachambuzi wanasema hatua hiyo inaweza kudhoofisha uwezo wa nchi zinazoendelea kuvutia wawekezaji kwa sera za kodi zinazowavutia.
“Tanzania inaweza kupoteza moja ya nyenzo chache tulizobakiza za kushawishi wawekezaji,” alisema afisa mwandamizi wa Wizara ya Fedha, kwa sharti la kutotajwa jina.
“Tayari tunakabiliwa na masharti kutoka kwa wakopeshaji tunapotoa vivutio vya kodi. Sasa kiwango cha chini cha kimataifa kitaweka mipaka zaidi.”
Makubaliano hayo yanayoongozwa na OECD yanatarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2026. Mawaziri wa fedha wa Afrika, wakiwemo wa Tanzania, wamesisitiza kuwa mapato yatakayopatikana yagawanywe kwa usawa na kwamba nchi zinazoendelea zisibaki wapokeaji wa sera zilizotungwa kwingine.
BRICS kama njia m,badala
Wakati huo huo, kundi la BRICS Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini linaendelea kujenga mifumo mbadala ya kifedha, ikiwemo New Development Bank (NDB) na BRICS Pay, mfumo wa malipo ya kidijitali unaolenga kupunguza utegemezi wa dola.
Nchi kadhaa za Afrika, zikiwemo Misri na Ethiopia, tayari zimeomba kujiunga na BRICS. Wataalamu wa sera nchini Tanzania nao wanafanya tathmini kimyakimya.
“Utofauti wa ushirikiano ni muhimu,” alisema Profesa Pantaleo Kessy wa UDSM. “Biashara yetu na China, India na Afrika Kusini tayari ni kubwa kuliko na Ulaya. Inapasa tuwe na mfumo wa kifedha unaoakisi uhusiano huo badala ya kufuata urithi wa kihistoria.”
Dhahabu: Nguzo ya uhuru wa fedha
Utajiri wa dhahabu nchini unazidisha umuhimu wa mjadala huu. Dhahabu kwa sasa inachangia takribani asilimia 45 ya mapato ya mauzo ya nje ya Tanzania, na Benki Kuu imeongeza akiba yake ya dhahabu kwa miaka ya hivi karibuni.
Wachumi wanasema mfumo wa akiba unaoungwa na dhahabu unaweza kusaidia kupunguza athari za misukosuko ya dola na kuimarisha uaminifu kwa shilingi.
Hata hivyo, wataalamu wanatahadharisha kuwa dhahabu si mbadala wa sera bora. “Dhahabu inaleta usalama, lakini si injini ya ukuaji,” alisema afisa mwandamizi wa Benki Kuu. “Akiba ni bima, si chanzo cha mapato. Changamoto ni kuunganisha dhahabu katika mkakati mpana wa kifedha.”
Hatua ya Kati: “Kutoegemea Upande wa Kifedha”
Kuelekea BRICS au mfumo wa dhahabu kungekuwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa. Tanzania ingeongeza uwezo wa kujitegemea, lakini pia ingeweza kukabiliwa na uhamishaji wa mitaji au ongezeko la gharama za mikopo iwapo wawekezaji wa Magharibi wangeona kama ishara ya upinzani wa kisiasa.
IMF na Benki ya Dunia bado ni wafadhili wakubwa wa miradi ya miundombinu na kijamii nchini. Mwaka 2025, IMF ilitoa Dola milioni 153 chini ya mpango wa RSF kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kujiondoa ghafla kwenye mikataba hiyo kunaweza kuvuruga bajeti na matumizi ya kijamii.
Kwa hivyo, wachambuzi wanashauri mkakati wa njia mbili: kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha za kikanda na BRICS, huku ikiendelea kushirikiana na washirika wa jadi.
“Uhuru haumaanishi kujitenga,” alisema Profesa Moshi. “Unamaanisha uwezo wa kuchagua bila shinikizo kile kinachoinufaisha nchi.”
Washauri wa sera mjini Dodoma sasa wanajadili wazo la “Kutoegemea Upande wa Kifedha,” likiwa ni mwendelezo wa falsafa ya Tanzania ya Non-Alignment katika enzi ya Vita Baridi. Lengo ni kutanua wigo wa washirika, sarafu na akiba ili kusiwe na kundi moja lenye mamlaka kamili ya kuamua mwelekeo wa taifa.
Kupitia sera hiyo, Tanzania inaweza kufanya yafuatayo:
-
Kuongeza akiba za dhahabu na sarafu zisizo za dola;
-
Kufanya mikataba ya kubadilishana fedha (swap lines) ndani ya SADC na Afrika Mashariki;
-
Kuelekeza fedha za miradi kupitia benki za BRICS na taasisi za kikanda;
-
Kuendelea kuwa mwanachama wa IMF na Benki ya Dunia lakini kudai masharti yenye kubadilika zaidi.
Mtazamo huu wa kivitendo ungeiweka Tanzania kama daraja kati ya mifumo ya kifedha duniani si kama chombo kinachochezewa ndani yake.
Hatimaye, mjadala kuhusu dola na kodi ya kimataifa unahusu zaidi siyo fedha tu, bali ni madaraka ya kisiasa. Udhibiti wa sarafu, mikopo na kodi ni sawa na udhibiti wa hatima ya taifa.
Kwa Tanzania, ambayo imekuwa kinara wa uhuru na ushirikiano wa Kiafrika, njia bora ni ile inayochanganya nidhamu ya kifedha na ujasiri wa kujitegemea.
Akiba ya dhahabu inaweza kujenga uaminifu; ushirikiano na BRICS unaweza kuongeza nafasi ya sera; lakini sarafu halisi ya uhuru ni uimara wa taasisi uwezo wa taifa kuamua, kutetea na kufadhili ajenda yake ya maendeleo.
Kadri mifumo ya kifedha ya Magharibi inavyozidi kukaza kamba, changamoto ya Tanzania ni kubaki wazi kwa dunia bila kumilikiwa nayo.