Dk.Biteko aahidi ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa Sekta ya Nishati
Balozi wa Marekani apongeza uteuzi wa Dk.Biteko
DAR ES SALAAM:Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Michael Battle, alipomtembelea leo, Septemba 13, 2023 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.
Dk. Battle amemtembelea Biteko kwa lengo la kumpongeza kwa uteuzi na majukumu yake mapya ikiwa ni pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kisekta baina ya nchi hizo mbili.
Katika mazungumzo yao Biteko ameeleza kuwa, Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati ikiwemo ya uzalishaji umeme pamoja na Mradi wa kubadili Gesi Asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG).
Dk.Biteko amesema, majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji wa Mradi wa LNG yako katika hatua nzuri na wataalamu wanaendelea kupitia vipengele vya mkataba huo ili kuhakikisha kila upande umeridhika.
Aidha amegusia kuwa upo uwezekano wa kurudia baadhi ya vipengele ili kuviboresha zaidi.
“Tunaendelea kupitia na kuboresha baadhi ya vipengele vya mkataba huu ili pindi utakapokuwa tayari uwe nyenzo ya kuhakikisha matarajio na manufaa ya mradi huu yanafikiwa,”alifafanua Dk. Biteko.
Naye Balozi Battle alimtaarifu Dk.Biteko kuwa zipo kampuni mbili za Kimarekani Astra Energy na Upepo Energy zenye lengo la kuwekeza nchini Tanzania kwenye eneo la uzalishaji umeme na tayari zimekwishawasilisha rasmi nia yao ya kuwekeza hapa nchini.
Akizungumzia kuhusu suala hilo Biteko ameahidi kufuatilia kuhusu wawekezaji hao kutokana na uhitaji mkubwa wa Nishati ya Umeme hapa nchini kwa sasa.