Dk Biteko aonya hasara upotevu wa maji

DAR ES SALAAM: UPOTEVU wa maji unaosababishwa na wizi umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa Mamlaka za Maji, baada ya kubainika kuwa maji yamepotea kwa asilimia 36, hali inayosababisha hasara ya takriban shilingi bilioni 114.1.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amebainisha hayo leo katika Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Maji kwa mwaka wa fedha 2023/24 uliofanyika jijini Dar es Salaam. Ameeleza kuwa fedha hizo zinazopotea zingeweza kutumika kuanzisha vyanzo vipya vya maji na kuboresha huduma kwa wananchi.
Mbali na upotevu wa maji, Dk. Biteko amesema changamoto nyingine ni uzalishaji wa maji usiokidhi mahitaji ya wananchi, pia amezitaja baadhi ya mamlaka zinazoongoza kwa upotevu wa maji ni Rombo (70%), Handeni (69%), Ifakara (56%) na Kilindoni (55%), huku Maganzo, Nzega, Kashuwasa na Bihalamuro zikiongoza kwa kudhibiti upotevu huo.

Aidha, Dk. Biteko ametoa wito kwa mamlaka zote za maji kushirikiana na sekta binafsi ili kutatua changamoto hizo na kuweka mikakati ya kupunguza upotevu wa maji ili kuepusha hasara kubwa kwa serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema mamlaka zinazohusika na upotevu mkubwa wa maji zinapaswa kuchukuliwa hatua kali kwa sababu fedha zinazopotea ni nyingi.
“Suala hili la utoaji wa taarifa za utendaji usiwe wa kawaida. Lazima tuwabainishe wasiofanya vizuri ili hatua zichukuliwe. Mkurugenzi sio suti, mkurugenzi ni utendaji. Badala ya kuzungumzia upotevu wa maji kwa asilimia pekee, tuziweke kwenye mfumo wa fedha ili kila mtu apate hisia za athari zake,” amesema Aweso.
Aweso ameipongeza EWURA kwa kusimamia suala la bili za maji na kuhakikisha upotevu wa maji unapungua.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof. Mark Mwandosya, amesema uwekezaji katika sekta ya maji una uhusiano mkubwa na sekta ya afya, kwani huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira husaidia kuzuia magonjwa ya mlipuko.
Mwandosya amerejerea Ripoti ya Taifa ya Takwimu ya mwaka 2022, inaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya taasisi za elimu ya msingi na sekondari zinapata maji safi na salama, hali inayowezesha wanafunzi kutumia muda wao kusoma badala ya kutafuta maji.



