NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko amesema kuwa kwa miaka yote wananchi wa Wilaya ya Bukombe wamekuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kiu ya maendeleo.
Amesema wananchi hao wana haki ya kuchagua kati ya maneno au maendeleo na wamekuwa wakitamani maendeleo kwa kuwa na shule, barabara na zahanati.
Dk Biteko amesema hayo wakati akifungua Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Bukombe zilizofanyika katika Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita.
“ Tunapozindua kampeni zetu tuna wajibu wa kuchagua maneno au maendeleo, tutashindanisha vyama kwa sera na kuonesha tuliyofanya kwa kipindi kilichopita. Tumekuja leo kuwaambia sisi tuko upande wa maendeleo na wengine wako upande wa maneno kama mwakilishi wenu nimekuja kuwaambia tuchague maendeleo, tuchague CCM,” amesema Dk Biteko.
SOMA: Dk Biteko ajiandikisha uchaguzi mitaa
Amesisitiza “Tuliwahi kupata viongozi wa chama kingine na sasa tuna wajibu wa kupima kati yao na CCM mabadiliko yako chama gani.”
Akielezea uandikishaji wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mtaa, amesema kuwa mwaka 2024 Bukombe imeandikisha wapiga kura 228,659 ikiwa ni rekodi ya juu katika mkoa na ukanda huo hali inayodhihirisha ushindi kwa CCM na hasa kutokana na utekelezaji wa ilani yake.
Halikadhalika, Dk Biteko amesema asilimia 70 ya vitongoji vina wagombea wa CCM huku vyama vingine vikishindwa kuweka wagombea.
“Novemba 27, 2024 wote tukapige kura tunatakiwa kumshukuru Rais Samia kwa upendo na kwa kufanya jitihada nyingi za kutujengea barabara, shule za msingi na sekondari, vyuo vya VETA, shule ya amali na mengineyo kwa haya yote twende tukawapigie kura wagombea wa CCM,” amesema Dk Biteko.