Dk. Feleshi: CMA, mahakama zisomane

DAR ES SALAAM: MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi ameitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuwa na mifumo inayosomana na mahakama ili kuweza kusaidia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama kwa kushirikiana na tume hiyo.

Wito huo ameutoa leo Julai 05, 2024 alipotembelea banda la CMA, katika banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba 2024) yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

SOMA: Wanasheria mnawajibu kuitetea Serikali- Mchengerwa

Dk.  Feleshi ameitaka CMA kutoa mafunzo kwa waajiri na waajiriwa ili kuweza kupunguza idadi ya migogoro ya kikazi inayotokana na ukosefu wa elimu, ili kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CMA, Usekelege  Mpulla amesema tume hiyo inatarajia kuanza matumizi ya mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao unaofahamika kama ‘Online Case Management System’ ambao utamuwezesha kila mwananchi kusajili mgogoro wake popote alipo.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya mkakati wa kuwafikia wananchi katika ngazi ya wilaya nchini.

Mpulla ameongeza kuwa, tayari CMA imejipanga  kuhakikisha huduma za tume zinapatikana katika ngazi ya wilaya na tayari CMA inatarajia kuanzisha tume inayotembea itakayowezesha wananchi  kupata huduma na haki kwa wakati.

Habari Zifananazo

Back to top button