DK JANE GOODALL: Historia yake kuhusu sokwe wa Gombe haitafutika

OKTOBA Mosi, 2025 ulimwengu ulipokea taarifa za kusikitisha za kifo cha Dk Jane Goodall baada ya miaka 91 ya safari yake ya maisha juu ya dunia.

Jane Goodall si jina geni miongoni mwa wapenzi wa uhifadhi wa mazingira na viumbe hai duniani. Tovuti ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania inamwelezea kama mwasisi wa taasisi hiyo na Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa, aliyekuwa mfano wa kuigwa wa ujasiri.

Dk Jane alifanya kazi bila kuchoka katika maisha yake yote akiibua uelewa kuhusu vitisho kwa wanyamapori, kukuza uhifadhi na kuhamasisha uwiano na uhusiano endelevu baina ya watu, wanyamapori na ulimwengu wa asili.

Dk Jane ambaye inaelezwa kuwa alifia usingizini, anatambulika ulimwenguni na hasa Tanzania kwa kutumia maisha yake akifanya utafiti wa sokwe katika Msitu wa Gombe unaopatikana Mto Gombe, Magahribi mwa Mkoa wa Kigoma.

SOMA: Aliyetafiti kuhusu sokwe afunguka wanavyopungua

Kwa miaka 65 alitumia muda wake mwingi kufanya utafiti kuhusu sokwe, ingawa sehemu ya mwisho ya maisha yake aliitumia katika harakati za kibinadamu, ustawi wanyama, viumbe hai na kukuza uhifadhi wa mazingira. Alikuwa na shauku ya kuwezesha vijana kushiriki katika uhifadhi na miradi ya kibinadamu na aliongoza miradi mingi ya kielimu kuhusu sokwe na wanyamapori.

Akiwa mzaliwa wa Hampstead, London nchini Uingereza kwa baba mfanyabiashara Mortimer Herbert Morris Goodall na mama mwandishi wa vitabu Margaret Myfanwe Joseph alipewa jina la Valerie Jane Morris-Goodall. Alianza mapenzi yake kwa wanyama akiwa mtoto mdogo na alisoma kwa bidii kuhusu ulimwengu wa asili.

Ndoto yake ilikuwa kusafiri hadi Afrika, kujifunza zaidi kuhusu wanyama na kuandika vitabu. Makala yaliyochapwa kwenye tovuti ya Taasisi ya Jane Goodall Tanzania yanabainisha kuwa, Dk Jane aliamua kufanya kazi kwa bidii kama mhudumu, ili aweze kuhifadhi fedha kutekeleza ndoto yake ya kufika Kenya.

Katika kutimiza azma hiyo, alishauriwa aonane na mwanasayansi wa masuala ya kale na mazingira, Dk Louis Leakey. Dk Leakey alimwajiri Dk Jane kama Katibu Muhtasi katika Makumbusho ya Taifa ya Nairobi na nafasi hiyo ikampa fursa ya kukaa pamoja na Louis na Mary Leakey katika eneo la Olduvai Gorge kutafuta mabaki ya kale.

Hiyo ilifungua mlango mwingine wa fursa, baada ya Dk Leakey kuona uvumilivu wa Dk Jane alimtaka aende Tanzania kufanya utafiti za sokwe katika Msitu wa Gombe. Julai 14, 1960 Dk Jane aliwasili katika Msitu wa Gombe kwa mara ya kwanza na hapo safari yake ya kipekee ikaanza.

Hiyo ilikuwa safari ya kuelewa tabia za sokwe kwa namna ya kipekee. Dk Leakey aliona kazi ya Dk Jane haitachukuliwa kwa uzito unaotakiwa, hivyo akaamua kumpeleka katika Chuo cha Newnham, Cambridge ambako alisoma masomo ya sayansi ya tabia za wanyama na kuhitimu shahada ya uzamivu.

Anafikia hatua hiyo baada ya kufanya utafiti uliobeba Kichwa ‘The Behaviour of Free-living Chimpanzees in the Gombe Stream Reserve’, yaani ‘Tabia za Sokwe Huru Katika Hifadhi ya Gombe’, (kwa tafsiri ya mwandishi) uliokamilika mwaka 1965.

Utafiti wake wa miezi mitatu ulibadilika kuwa mpango wa kipekee wa utafiti uliodumu kwa miongo kadhaa na bado unaendelea kutumika hadi leo. Kwa mujibu wa makala hayo, Dk Jane alifunga ndoa mara mbili. Ndoa ya kwanza ilikuwa baina yake na mpiga picha za mazingira na wanyamapori, Hugo van Lawick, raia wa Uholanzi lakini hata hivyo, walitalikiana mwaka 1974.

Kisha akaoana na Derek Bryceson aliyewahi kuwa mbunge na waziri katika serikali ya Tanganyika lakini pia alikuwa Mkurungezi wa Hifadhi za Taifa Tanzania. Katika uhai wake, Dk Jane ameandika zaidi ya vitabu 27 vya watoto na wakubwa na kushiriki makala na filamu mbalimbali.

Mwaka 2019 Jarida la National Geographic lilianzisha maonesho yaliyopewa jina la ‘Becoming Jane’ yaani, maonesho ya safari yaliyolenga kuelezea maisha yake ya kazi. Kitabu chake cha hivi karibuni ‘The Book of Hope: A Survival Guide for Trying Times’ yaani ‘Kitabu cha Matumaini: Mwongozo wa Kuishi Katika Nyakati za Majaribu’ kimetafsiriwa katika zaidi ya lugha 20 duniani.

Aliwahi kupata tuzo mbalimbali na kupewa ubalozi wa amani wa Umoja wa Mataifa mwaka 2002. Miaka miwili baadaye alipewa heshima ya kipekee katika Jumba la Kifalme la Buckingham na kufanywa kuwa Kamanda wa Agizo la Dola ya Uingereza.

Aidha, vyanzo vinasema Dk Jane aliwahi kupewa tuzo ya Mpatanishi wa Uhuru wa Rais wa Marekani, Tuzo ya French Légion D’honneur ya Ufaransa, Medali ya Benjamin Franklin, Tuzo za Fahari za Japan Kyoto na nyingine nyingi.

Mwaka 1977, Dk Jane alianzisha Taasisi ya Jane Goodall akilenga kusaidia utafiti katika Msitu wa Gombe. Kwa sasa taasisi hiyo ina ofisi 25 zinazofanya miradi anuai duniani. Mwaka 1991, Dk Jane alianzisha mradi alioupa jina la ‘Roots & Shoots’, ulioshirikisha vijana wa rika zote katika masuala ya kibinadamu na mazingira.

Juhudi za mradi huo zilianzia kwa wanafunzi wa shule za sekondari 12 za Mkoa wa Dar es Salaam na leo mradi huo unafanya kazi katika nchi 75. Wanachama wanaoshiriki mradi huo wanawezeshwa katika kuweka mabadiliko chanya kwa wanyama, mazingira na jamii za wenyeji katika maeneo yao.

Hakuishia hapo, kwani mwaka 2017 alianzisha Mfuko wa Jane Goodall Legacy uliolenga kuhakikisha kuna mwendelezo wa shughuli alizoanzisha katika maisha yake ya kazi.

Kupitia maisha yake, Dk Jane alivutia vizazi vya wanasayansi, kuleta matumaini kwa watu wasiohesabika na kufanya ulimwengu ukumbuke kwamba kila mmoja wetu anaweza kufanya tofauti kila siku na ni juu yetu kulingana na aina ya tofauti tunayofanya.

Ni wazi kuwa urithi wa kazi zake unaonekana na kuendelezwa katika utafiti unaoendelea kwenye msitu wa Gombe Tanzania, kazi ya hifadhi za sokwe za Eden nchini Afrika Kusini na Tchimpounga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na Mradi wa Roots & Shoots unaowezesha vijana kushiriki katika mipango ya jamii, wanyama na mazingira.

 

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa mtandao

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button