Aliyetafiti kuhusu sokwe afunguka wanavyopungua

DAR ES SALAAM; MTAFITI mwandamizi aliyepaisha Hifadhi ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma kwa kutafiti kuhusu maisha na tabia za sokwe, Dk Jane Goodall ametimiza miaka 90, huku utafiti wake kuhusu wanyama hao ukitimiza miaka 64.

Dk Goodall chini ya taasisi yake ya Jane Goodall (JGI) alifanya utafiti huo tangu mwaka 1964 na kuufanya kuwa utafiti wa muda mrefu zaidi Tanzania.

Hata hivyo, kupitia utafiti huo aliipaisha hifadhi ya Gombe na kutambulika kote duniani kama hifadhi yenye sokwe mtu wengi nchini.

Advertisement

Akizungumza leo katika Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), amesema wakati anaanza utafiti huo, idadi ya sokwe mtu katika hifadhi hiyo walikuwa kati ya 120-150, lakini sasa wamepungua kufikia 85 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo milipuko ya magonjwa na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye hifadhi hiyo.

Kuelekea siku ya Sokwe duniani inayoadhimishwa Julai 14, kila mwaka, ameshauri kulindwa kwa mnyama huyo adimu duniani.

Amesema JGI inashirikiana na serikali za mitaa kushughulikia matishio ya uhifadhi kwa kutumia sayansi na teknolojia sambamba na kutoa elimu kuhusu usimamizi wa maliasili na mazingira.

SOMA:https://habarileo.co.tz/jane-goodall-apewa-barabara-kigoma-ujiji/

Mtafiti huyo amesema kadri idadi ya binadamu inavyoongezeka na misitu inapungua, hivyo idadi kubwa ya sokwe hugawanyika na kupunguza utofauti wa kijeni na uwezekano wa kuishi kwa muda mrefu kwa kila jamii.

‘’Taasisi ya Jane Goodall inaamini kwamba njia bora ya kulinda makazi yenye afya ni kuzingatia vitendo ambavyo sio tu vinalinda wanyama walio hatarini na makazi yao, lakini pia kunufaisha watu wa eneo hilo ambao maisha yao yanategemea mazingira bora,’’ ameeleza Dk Goodall.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu amesema kuwa utafiti huo wa sokwe ni wa muda mrefu toka ulipoanzishwa na mtafiti mwandamizi na muanzilishi wake Dk Goodall ambaye amefikisha miaka 90 sasa.

“Leo nimetembelewa na watafiti kutoka taasisi ya Goodall wanaofanya utafiti wa sokwe utafiti huu ni mkubwa na wa muda mrefu ambao umetoa matokeo ambayo yamebadili taswira ya mahusiano ya binadamu na wanyama kwa dunia nzima,” amesema Dk Nungu.

Ameeleza kuwa utafiti wa sokwe ni miongoni mwa tafiti mbalimbali ambazo wanazitolea vibali na hata kuzifadhili moja kwa moja .

‘’Dk Goodall na timu yake wamekuja kushukuru sababu mtafiti huyu amefikisha miaka 90 ya kuzaliwa, lakini pia anashukuru Costech kwa kutoa vibali vya utafiti nasi tumekuwa tukiangalia wanavyoendelea na tumeona matokea ya utafiti wao umeleta mahusiano kati ya binadamu na wanyama,” amesisitiza.