Wadau wajadili mwelekeo wa Tanzania kwenye utalii

ARUSHA: Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii katika Destination Tanzania Stakeholders Forum 2026 iliyofanyika jengo la Ngorongoro, Arusha, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuitangaza Tanzania na kuongeza ushindani wa sekta ya utalii duniani.

Jukwaa hilo liliwakutanisha wawakilishi kutoka serikalini, sekta binafsi, vyama vya utalii, waongoza watalii, mahoteli, mashirika ya ndege, taasisi za uhifadhi, washirika wa maendeleo pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo kujadili fursa, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuendeleza Destination Tanzania.

Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru, alisema mafanikio ya kuitangaza Tanzania hayawezi kufikiwa na taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza duniani kwa utalii.

Katika mkutano huo, TTB iliwasilisha Destination Tanzania Portal, jukwaa la kidijitali linalolenga kuunganisha taarifa za utalii, kuongeza mwonekano wa vivutio vya Tanzania na kuboresha upatikanaji wa taarifa kwa watalii na wadau wa sekta hiyo. Washiriki walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu maboresho yanayoweza kufanywa ili mfumo huo uwe na tija zaidi kwa watumiaji.

Mbali na uwasilishaji huo, wadau walipata nafasi ya kutoa maoni kuhusu kampeni za masoko ya utalii, ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya kimataifa, matumizi ya majukwaa ya kidijitali, maandalizi ya matukio makubwa ya kimataifa pamoja na namna ya kuendelea kujenga taswira chanya ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

TTB ilieleza kuwa maoni yote yaliyokusanywa yatazingatiwa katika kuboresha mikakati ya utangazaji wa Destination Tanzania na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii, uwekezaji na mchango wa utalii katika uchumi wa taifa.

Jukwaa hilo limehitimishwa kwa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana katika kuitangaza Tanzania kama kivutio bora cha utalii duniani kupitia ubunifu, ushirikiano na mshikamano.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button