Dk. Jasmin awashauri wanawake kupima afya ya uzazi

DARESSALAAM : DAKTARI Bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya Medinova, Dkt. Jasmin Kallarakampoyil, amewashauri wanawake kuwa na tabia ya kupima afya zao za uzazi ili kuepukana na matatizo ya ugumba na magonjwa ya zinaa.
Akizungumza na HabariLeo kuhusu hali ilivyo kwa wanawake wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Jasmin amesema tatizo kubwa ni wanawake wengi kutokuwa na utamaduni wa kufuata ushauri wa madaktari kuhusu afya zao za uzazi.
Amesema kuwa wengi wao wamekuwa wakiamini zaidi katika tiba za kienyeji na tiba za virutubisho vya asili badala ya kutafuta huduma za kisasa kutoka kwa wataalamu wa afya.
“Wanawake wengi huchukua dawa za kienyeji au virutubisho ili kutibu matatizo ya uzazi na magonjwa mengine ya zinaa bila kuzingatia ushauri wa madaktari,” alieleza Dkt. Jasmin.
SOMA: Wizara ya afya yaingia ushirikiano afya ya uzazi
Dkt. Jasmin ameongeza kuwa hatua hii inachangia matatizo mbalimbali, ikiwemo wanawake kuharibu vizazi, kushindwa kupata ujauzito, kupata magonjwa mapya, na wengine kupoteza maisha kutokana na kutokuwa na huduma bora za afya.
“Hivyo, ni muhimu kwa wanawake kuwa na tabia ya kupima afya zao za uzazi mara kwa mara ili kujua hali zao za kiafya na kuepuka matatizo yasiyohitajika,” alisema Dkt. Jasmin.



