Dk Jingu: Serikali imeweka fursa, vijana jitambueni

DAR ES SALAAM: Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk John Jingu amesema serikali imeweka mazingira wezeshi ya kukopa kwa vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi .
Hayo ameyasema leo jijini Dar es Salaam kwenye tamasha la twenzetu kwa Yesu liliandaliwa na Upendo Media ambapo ameongezea kwa kusema vijana wawe nguvu chanya na chachu ya maendeleo kwa taifa kwani linawategemea.

Aidha, Jingu amewahimiza vijana wajitambue ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha kwani serikali imeweka fursa mbalimbali za uwezeshaji kwa ajili yao ikiwemo mitaji na riba yenye masharti nafuu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule amesema kupitia tamasha hilo litawajenga vijana wengi hivyo wilaya ya kinondoni ina fedha maalumu zilizotengwa asilimia nne kwaa ajili ya vijana kukopa ili wajiendeleze.

Awali akiongea Mkurugenzi wa Upendo Media Neng’ida Johanes amesema lengo kuu la kuandaa kongangamo hilo ni kuwaleta vijana pamoja kuwafunza mambo mema yanayompendeza Mungu pamoja na kufata maadili mema.
Nao Vijana walioshiriki kongomano hilo Ebenezer Matimbwi na Diana Titlya wamesema tamasha hilo kwao linawajenga kiroho pamoja na kimaadili kwa jamii inayowazunguka.



