Dk.Migiro: Mwanamke Anayeandika Historia Kwenye Medani za Siasa na Diplomasia

KATIKA medani ya siasa, diplomasia na utawala wa Tanzania na hata nje ya mipaka ya Tanzania, jina la Dk Asha-Rose Migiro linaendelea kung’ara kwa heshima na uzito wa kipekee. Katika historia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), jina la Dk Migiro litabaki katika kitabu cha kumbukumbu na historia kama mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa ngazi ya juu ndani ya chama hicho.
Ndiyo, ni Dk Asha-Rose Migiro aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu wa CCM kuchukua nafasi ya Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye ni mgombea mwenza wa mgombea wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan. Mwanamama huyu si mpya katika majukwaa ya uongozi, nyota yake imeng’ara tena katika majukwaa ya kisiasa akiianza safari ya kukitumikia chama chake katika nafasi ya juu hasa wakati huu wa Uchaguzi Mkuu 2025.
Dk Migiro ni kiongozi aliyejijengea sifa ya weledi, uhodari na uwezo wa kuchambua changamoto kwa mtazamo wa kimkakati, sifa zinazomfanya awe wa kupigiwa mfano kwa wanawake wengi wa kiafrika. Uwezo wake wa kitaaluma, kisiasa, na diplomasia ndiyo unaompamba mwanamama huyu mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya kidiplomasia ya kimataifa hasa kutokana na nafasi alizowahi kuzitumikia hapo nyuma.
Dk Migiro ambaye kitaaluma ni mwanasheria alizaliwa Julai 9, 1956 na taaluma yake ilimpeleka kwenye siasa mwaka 2000 na baadaye kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Waziri wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto tangu 2000/2005 na baadaye 2006/2007 Waziri wa Mambo ya Nje.
Februari 2007, Dk Migiro aling’ara kimataifa baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa chini ya Katibu Mkuu wa wakati huo, Ban Ki-moon ambayo ni nafasi ya juu zaidi kuwahi kushikiliwa na Mtanzania katika historia ya chombo hicho na alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2012, na kuacha alama ya kipekee katika uongozi wa kimataifa hasa kwenye ajenda za maendeleo, amani na usawa wa kijinsia kwa wanawake.
Desemba 12, 2013 mpaka Julai 2015 aliteuliwa kuwa mbunge katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na baadaye Januari 2014 mpaka Novemba 2015 alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria katika kipindi hicho, Dk Migiro alihusika kwenye masuala ya mageuzi ya kisheria akitoa mchango mkubwa kwenye mijadala ya katiba mpya na misingi ya haki.
Mwaka 2016-2023 alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, nafasi aliyoitumia kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza na katika kipindi chake, Tanzania ilishuhudia ongezeko la wawekezaji kutoka Uingereza sambamba na mikakati ya kidiplomasia iliyoimarishwa katika Jumuiya ya Madola.
Mwanamama huyo pia aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria mwaka 2011-2016 na amekuwa kiungo muhimu katika sekta ya elimu ya juu na sera za kitaifa za maendeleo. Pia, aliwahi kuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1981- 2000. SOMA: Migiro: CCM itashinda kwa kishindo
Kwa sasa Dk Migiro pia, ni Mwenyekiti wa timu ya uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo Rais Samia aliizindua Julai 17, mwaka huu. Kwenye mapokezi yake hivi karibuni katika ofisi za CCM Dodoma, Dk Migiro alisisitiza dhamira yake ya kujenga mshikamano ndani ya chama, kudumisha maadili ya msingi pamoja na kusimamia majadiliano ya kimaendeleo kwa uwazi na ushirikishwaji.
Pia, alisisitiza nafasi ya vijana na wanawake katika kujenga taifa jipya lenye dira. Anasema anaona fahari kurithi majukumu makubwa yaliyoachwa na mtangulizi wake Dk Nchimbi na kusisistiza umoja na ushirikiano kwa wanachama wengine. “Katibu Mkuu (Dk Nchimbi) kama ni msitu ameufyeka na mimi nakuja kupita kwenye njia iliyonyooka nikiwa na wazee, vijana na wana CCM, nikiwa na imani tutashinda na ushindi ni lazima”.
Anasema nafasi yake ya katibu imetokana na ushirikiano wa wanachama wakati akiwa katika sekretarieti na kuaminiwa kwa mtangulizi wake kwa sababu wanachama ndio mtaji wa chama hicho. “Tuko tayari kwa kuanza mapambano na kuhakikisha tunakipatia ushindi wa kishindo chama chetu naishukuru sana imani mliyonionesha pamoja tutaongoza chama chetu kipenzi kufikia mafanikio katika uchaguzi ujao.”
Anasema kama Katibu Mkuu yupo tayari kwa mapambano ya kutetea chama na kukipa ushindi ili wagombea wapate ushindi mnono na hata wale wa majimboni, na madiwani waibuke kidedea. “Tunakwenda kuhakikisha ushindi kwa rais na mgombea mwenza wake, wabunge na madiwani tunapata ushindi mnono na nafasi zote tutaibuka kidedea.”
Mchango wa Dk Migiro ndani ya CCM Uteuzi wa Dk Migiro ndani ya CCM ni ishara kuonesha chama hicho kikongwe kinasimamiwa na nguvu mbili za kike; Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dk Migiro.
Dk Migoro ni ushahidi wa jinsi chama hicho kilivyoanza kutekeleza kwa vitendo dhana ya usawa wa kijinsia na kuwaamini wanawake katika nafasi nyeti za maamuzi. Kupitia uzoefu wake mkubwa katika utawala wa ndani na nje ya nchi, Dk Migiro anatarajiwa kuleta mtazamo wa kimkakati ndani ya CCM kwa kuimarisha taasisi, kusimamia nidhamu ya wanachama na kuendesha chama kwa misingi ya kitaasisi.
Kadhalika nafasi hiyo inampa fursa kubwa ya kuongoza mijadala kuhusu sera, mikakati ya maendeleo na maono ya kisiasa ya chama na kuunganisha ajenda za chama na dira ya taifa, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 anayoiongoza kwa sasa.
Pia, kutokana na uzoefu wake wa kidiplomasia, Dk Migiro ana nafasi ya kukiunganisha chama na vyama rafiki vya kimataifa, taasisi za maendeleo na jumuiya za kimataifa kwa ajili ya ushirikiano wa kimkakati unaolenga masilahi ya chama na taifa. Dk Migiro alitoa mchango mkubwa alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), ikiwemo kusimamia mipango ya mageuzi ndani ya UN na alihusika katika kuimarisha utendaji wa umoja huo kwa kusimamia mageuzi ya kiutawala na uwajibikaji ndani ya UN, kuhakikisha taasisi hiyo inafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kwa matumizi sahihi ya rasilimali.
Pia, Dk Migiro amesaidia kuweka misingi ya ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo kwani aliongoza mikutano mingi kuhusu ushirikiano wa kimataifa katika kutokomeza umasikini, kusaidia nchi masikini kupata teknolojia na kuongeza misaada ya maendeleo. Pia, alisaidia kuunganisha sekta binafsi, serikali na mashirika ya kiraia katika kufanikisha malengo ya kimataifa ya maendeleo.
Unapozungumzia ajenda ya usawa wa kijinsia, Dk Migiro ana mchango mkubwa kwa kusimamia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu katika uwezeshaji wa wanawake kwa kusukuma mataifa mengi kuweka sera na hatua madhubuti za kupunguza ukatili wa kijinsia, kuongeza elimu kwa wasichana na kuimarisha ushiriki wa wanawake katika siasa nchini